Dondoo

Demu ajuta kumtema mpenzi wa chuoni

January 8th, 2019 1 min read

Na Leah Makena

Kangaru, Meru

Kidosho wa hapa alifokewa vikali na jamaa aliyekuwa mpenzi wake chuoni kwa kutaka kumrudia baada ya kumtema kwa miezi minne.

Jamaa na kidosho walikutana chuoni na baada ya kufahamiana wakawa wapenzi. Barobaro alijitwika jukumu la kushughulikia mahitaji ya kidosho kupitia biashara ndogo aliyokuwa akiendesha jioni baada ya masomo.

Inasemekana kuwa familia ya mwanadada haikuwa na uwezo wa kifedha ila hilo halikusumbua mrembo kwani alikula na kuvaa vizuri kupitia juhudi za mpenzi wake aliyekuwa amejitolea kumtunza.

Masaibu yalianza walipokuwa katika likizo ya miezi minne kidosho alipokatiza mazungumzo ghafla jambo lililomtatiza jamaa.

Licha ya jamaa kufanya juhudi za kusaka mwanadada, hakufanikiwa kwani alielezwa kuwa mrembo alikuwa kiguu na njia akisakata densi na kushiriki kwenye sherehe na waume waliokuwa wakimpa pesa, habari ambazo jamaa alithibitisha na kughadhabika pakubwa.

Baada ya kimya cha miezi minne, kidosho alishangaza kwa kumpigia simu jamaa akitaka kumshawishi waanze kuishi pamoja chuoni. Hapo ndipo polo alipandwa na mori na kuzima mwanadada.

“Baada ya miezi minne sasa ndio unanikumbuka kwa sababu unataka nikutunze chuoni? Kama ulikuwa na haja na mimi mbona uliniweka kando kwa miezi hiyo yote? Najua mchezo wako na sitakubali unitumie vibaya. Mwaka huu pambana na hali yako ama waliokuwa wakikupeleka deti wakati wa likizo wakushughulikie,” polo alifoka.

Juhudi za kidosho kuomba msamaha hazikufaulu na akabaki njia panda asijue afanye nini kwa sababu ukweli ni kuwa ni jamaa aliyekuwa akimfadhili chuoni na aliokuwa akila fuska nao hawakuwa tayari kumsaidia kuendelea na masomo.