Dondoo

Demu ajuta kutema jamaa ‘msoto’

September 15th, 2020 1 min read

Na Mirriam Mutunga

KATHWANA, THARAKA NITHI

MWANADADA mmoja kutoka hapa alidondokwa na machozi mpenzi wake wa awali alipomuoa dada yake na kumjengea nyumba ya kifahari.

Duru zinasema demu alimtema jamaa huyo baada ya kuzozana na kumsimanga akidai kwamba hakuwa na mali ya kumtunza na kufurahisha mke.

“Alimuacha kwa dharau na kumtusi alipodanganywa na mwanamume mwingine aliyekuwa na pesa,” alisema mdokezi. Inasemekana baada ya demu kumrushia jamaa cheche za maneno, jamaa alianza kumtongoza dada yake ambaye alimkubali bila masharti.

Jamaa naye alifanikiwa katika biashara akawa tajiri huku demu aliyemuacha akipigwa teke na jombi aliyemdanganya. Majuzi, demu huyo alishangaa ‘Ex’ wake alipofika kwao nyumbani na kutangaza kwamba alikuwa anataka kuoa dada yake.

“Jamaa alikaribishwa na baba wa demu huyo kwa furaha na kuelezea azma ya kutaka kuoa dada wa Ex wake,” alisema mdokezi. Inasemekana demu alipigwa na butwaa jamaa alipokubaliwa kuoa dada yake na kupandwa na hisia kali na kuanza kulia huku akimrai jamaa amsamehe.

“Najuta sasa. Nakuomba unisamehe. Ni shetani alikuwa ananitumia siku niliyokutusi na kukuacha,” demu alimwambia jamaa huku akiwa amepiga magoti. Mdokezi asema jamaa alimsamehe demu Lakini akamwambia kwamba hangemkubali tena.

“Ni sawa nimekusamehe lakini sasa siwezi kurudiana na wewe. Sasa nampenda dada yako na mzee amenikubali nimuoe. Tayari nimejenga nyumba ya kifahari na niko tayari kuishi na familia yangu. Usiwe na wasiwasi utafanikiwa kumpata mwanaume mzuri wa kukuoa,” jamaa alimwambia demu.

Ilibidi mzee kumtuliza demu ili aache kuangua kilio.