Dondoo

Demu alazimisha awe mke wa pili

August 30th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

GANZE, KILIFI

DEMU aliyewekwa kinyumba na jamaa mtaani hapa na kupata mimba, alikataa kuondoka mke wa jombi alipofika na akataka aolewe mke wa pili.

Kizaazaa kilizuka pale mke wa jamaa aliporejea baada ya kusikia fununu kwamba alikuwa ameoa.

“Jamaa alitengana na mkewe na akamweka mwanadada kinyumba. Mkewe aliposikia mumewe alikuwa na mke mwingine, alirudi bila taarifa akamkuta akisafisha nyumba,” alisimulia mdokezi. Wawili hao walianza kurushiana maneno makali yaliyoalika majirani.

“Kila mmoja aliropokwa akidai alikuwa kwake,” aliarifu mdokezi, akisema majirani walikuwa wakiamua wawili hao wasipapurane.

“Hii ni nyumba yangu. Tulitengana na mzee wangu lakini sasa nimerudi kwangu, ondoka urudi ulikotoka, mwenye nyumba amefika,” mama alimfokea kipusa.

Hata hivyo, mwanadada alikaa ngumu na kufungua moyo wake.

“Kwa taarifa yako nina mimba yake, siondoki ng’o,” alifoka demu.

Kizaazaa kilipokuwa kikiendelea, jombi alitoka kazini na kushangaa kuona watu wakiwaamua.

“Mimi ni mwenye nyumba hii, wewe ulienda kwenu nikamleta huyu anisaidie,” jombi alimwambia mkewe.

“Na mimi ni mkeo wa ndoa na hapa ni kwangu, nimerudi na sibanduki,” alifoka mkewe.

“Hapa pia ni kwangu na tayari nina mimba yake,” mwanadada aliropokwa.

Wazee walitumia hekima kuwatuliza, jombi wakamwambia jamaa akubali mkewe arejee. Demu aliitikia wito wa wazee shingo upande huku jombi akishauriwa akubali kuwa na wake wawili.

“Itabidi huyu naye awe mkeo na ukimkataa mkeo utaleta balaa,” wazee walimwelezea jombi.

Ilibidi jombi ashauriane na mkewe kuhusu uke-wenza na walipoafikiana demu aliridhika, akakodishiwa nyumba kwingine.