Dondoo

Demu aliyeachika ajiwekea azimio la kutopenda tena

January 4th, 2024 1 min read

NA JANET KAVUNGA

LIKONI, MOMBASA

MWANADADA wa hapa ametangaza kuwa kuanza mwaka 2024 ameazimia kusahau wanaume baada ya kutemwa na kalameni aliyewekeza nguvu, muda na rasilimali kufanikisha uhusiano wao.

Demu alisema kuachwa na jamaa huyo kulimvunja moyo akachukia mapenzi na kamwe hatakubali mistari ya mwanamume yeyote.

“Ninahisi ulimwengu wa mapenzi kwangu umefika mwisho. Nimeamua kuishi singo katika muda ambao Mungu atanijilia kuwa hai,” demu alisema kwenye ukurasa mmoja wa mtandao wa kijamii wa wanawake kujadili masuala ya mapenzi.

Hata hivyo, wanachama wenzake walimshauri atulize hasira na kujipatia muda wa kupona baada ya kuachwa.

“Jipe muda, utachangamkia mapenzi tena,” kipusa mmoja alimweleza.