Dondoo

Demu aliyeteka mdosi wake ajuta kujigamba

November 16th, 2018 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

Masii, Mwala

KIPUSA anayefanya kazi katika duka moja la jumla mjini hapa alijipata pabaya kwa kujigamba kwamba alikuwa mpango wa kando wa mdosi wake.

Hii ni baada ya wenzake kutilia shaka uhusiano wa mwanadada huyo na bosi wao kwa sababu haikuwa kawaida kwa mwajiri wao kushirikiana na wasichana kazini kwa kuwa ana mke na watoto.

Penyenye zinasema demu huyo tunayefahamishwa amejaliwa umbo linalofanya wanaume kuvunjika shingo wakimtazama, aliajiriwa majuzi na mdosi akawa anamkazia macho na kumpa majukumu ambayo kwa kawaida hakuwa akiwapa wafanyakazi wengine.

Siku ya kioja, wenzake waliamua kuuliza demu huyo uhusiano wake na mdosi wao naye hakusita kuwaambia ukweli.

“Wewe, mbona umekuwa karibu na mdosi sana na inaonekana kuna kitu kinachoendelea. Boss ni mtu ambaye huwa anajiheshimu sana na hakuna mtu hapa aliwahi kumkaribia sana kama wewe,” kipusa mmoja alisema.

“Msinishangae kinachofanya mdosi kunipenda. Natumia ujanja na sura yangu kumpagawisha. Nyinyi mtabaki kulalamika tu ilhali nimemuingiza katika boksi yangu. Sifanyi kazi hii kwa sababu ninaipenda. Ninayempenda ni boss na tayari amenikubali. Nilimpangawisha kwa kutumia urembo wangu. Jitazameni mlivyochakaa,” demu aliendelea kujitapa mbele ya wenzake kazini .

Yasemekana wenzake walikasirika kipusa alipowadunisha na wakaamua kumkemea.

“Hautaharibu boss wetu ambaye amekuwa mtu mwenye heshima. Shetani wewe!Tutamtetea. Kuanzia leo usimkaribie mdosi hata kidogo,” wenzake walimuonya.

Inasemekana kipusa alikerwa na maneno ya wenzake na kuanza kuwarushia cheche za matusi. Hata hivyo wenzake walitisha kumchapa.

Yadaiwa tangu siku hiyo demu huyo aliacha kujipendekeza kwa mdosi.