Dondoo

Demu amzaba kofi landilondi kwa kukatalia deposit

May 20th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA
ZIMMERMAN, NAIROBI

KIZAAZAA kilizuka kwenye ploti moja mtaani hapa baada ya kipusa kumzaba kofi landilodi alipokataa kumrudishia deposit yake alipokuwa akihama.

Inasemekana kipusa aliudhika sana na uamuzi wa landilodi wa kukataa kumrejeshea pesa zake alipokuwa akihama.

Duru zinasema kipusa alipohamia katika ploti hiyo, alipewa masharti ambayo alifaa kutimiza ndiposa aruhusiwe kuishi hapo.

Alifaa kulipa renti, pesa za stima, pesa za maji na pesa nyingine kiasi sawa na renti ili kugharamia uharibifu wowote wa nyumba ambao ungetokea akiishi kwa nyumba.

Inasemekana kipusa alitimiza masharti hayo kwa makubaliano kwamba atarejeshewa hela zake zote iwapo nyumba haitakuwa na uharibifu wowote.

Habari zilizotufikia zinasema siku ya mrembo kuhama ilipofika alimuita landilodi kuikagua nyumba ili kutathimini kama kuna uharibifu wowote. Inadaiwa nyumba ilikuwa haina kasoro yoyote.

“Mimi napanga kuhama leo jioni. Hata gari la kubeba mizigo yangu ndilo lile. Naomba unirejeshee deposit yangu,” kipusa alimueleza landilodi.

Kulingana na mdokezi wetu, landilodi alimueleza kipusa angojee hadi mwisho wa mwezi ndiposa ampe hela zake.

“Sina hela za kukupa leo. Mambo ni mawili; ungojee mwisho wa mwezi ama uendelee kuishi kwa kwa nyumba lakini utumie deposit yako,” landilodi alimueleza kipusa.

Penyenye zinasema kipusa alianza kumzomea landilodi huku akiapa lazima apate.

“Wewe huna huruma hata kidogo. Wakati mmoja nusura unirushe nje nilipokupa renti nusu. Leo hii unaniambia ningojee hadi mwisho wa mwezi. Hayo hayawezekani,” kipusa aliapa.

Inadaiwa landilodi aliamua kunyamaza na kuondoka . “Wewe bwana acha madharau. Leta hela zangu haraka. Hata unafaa kunirudishia hadi za stima kwa sababu nyumba yangu umeme ulikuwa ukipotea kila mara,” kipusa alimfokea landilodi.

Alipoona landilodi amejitia hamnazo, kipusa alimfuata mbio na kuanza kumpa kichapo huku wapangaji wengine wakimshabikia.