Dondoo

Demu ashtua walevi kulilia kileo kilabuni

April 2nd, 2018 1 min read

NA JOHN MUSYOKI

KIVANDINI, MATUU

DEMU wa hapa alishangaza watu kilabuni alipoangua kilio baada ya mpenzi wake kudinda kumnunulia pombe.

Taarifa mtaani zinasema wapenzi hao walikuwa kilabuni kujiburudisha wakati jamaa alipobadilisha nia ya kununulia demu chupa mbili za pombe alivyokuwa ameahidi.

Kisanga kilitokea kalameni alipoagiza chupa mbili za soda hali iliyomshtua demu  na akaanza kufoka.

“Yaani unaagiza soda badala ya pombe. Kwani wewe ni kigeugeu kama kinyonga. Uliniambia msimu huu wa pasaka utaniburidisha kwa  pombe chupa mbili. Ahadi ni deni, sinywi soda hata ukiagiza,” demu alisema huku machozi yakimtoka.

Kalameni  alilaumu demu wake kwa kupenda mvinyo kupindukia.

“Wewe ni mwanamke sampuli gani? Badala ya kupenda chakula unatamani pombe. Kama pombe imekolea mwilini itabidi unywe maji upunguze kiu chako. Sitakununulia pombe na ukiendelea kuleta kisirani nitakuonyesha cha mtema kuni,” kalameni alisema.

Hata hivyo demu alizidi kulilia pombe.  “Wewe sio mtu mzuri. Una uwongo mwingi na sikuamini. Kwa nini umeamua kuniruka na uliniahidi pombe,” demu alilalamika.

Kamsa ya demu huyo ilivutia watu hadi ikabidi waende kujua kilichokuwa kikijiri.

Mteja mmoja aliyekuwa akinywa pombe aliposikia demu alikuwa analilia pombe, alimpa chupa kadhaa lakini alikiona cha mtema kuni kalameni alipomrukia kwa mateke huku akimlaumu kwa kumpa mkewe kileo.

“Bure kabisa, nani amekupa ruhusa ya kupatia mke wangu pombe. Kwenda kabisa. Ukijaribu kucheza na akili yangu nitakunyorosha kabisa,” kalameni alichemka.

Watu Walimlaumu mteja huyo kwa kuingilia mzozo wa mtu na mkewe na wakimtaka ajitenge kabisa. Baadaye kalameni alimshika demu mkono na kumburuta huku akimfokea vikali.

Haikujulikana kilichojiri baada ya wawili hao kufika nyumbani.

…WAZO BONZO…