Dondoo

Demu asusia ‘shopping’ baada ya jamaa kutamka neno moja la kumdhalilisha

February 26th, 2024 1 min read

MALINDI MJINI

Na JANET KAVUNGA

Kioja kilishuhudiwa nje ya duka moja mjini hapa, demu alipomuachia mpenzi wake bidhaa alizomnunulia walipotofautiana wakielekea kuingia gari.

Wawili hao walifanya ‘shopping’ kwa furaha huku demu akichagua bidhaa alizotaka na jamaa akazilipia.

Waliondoka kuelekea walikoegesha gari huku wakionekana wenye furaha kabla ya jamaa kutamka jambo lililomkasirisha demu, akasimama na kumtazama kisha akalipuka kwa hasira.

“Unaweza kunifikiria hivyo. Unadhani nitakubali unidhalilishe kwa sababu ya ‘shopping’. Kaa nayo upeleke kwako. Siitaki,” demu alifoka na kuondoka akamuacha jamaa akiwa ameduwaa.

Inasemekana jamaa alichukua bidhaa akaweka kwa gari na kuondoka.

***

Mapolo wasusia kazi walipobaini kati yao kulikuwa na jasusi wa bosi

SOIT, TRANSMARA

NA NICHOLAS CHERUIYOT

Vibarua kwenye shamba la mahindi eneo hili walisusia kazi walipojua barobaro mmoja alitumwa huko ili wasiibe mazao ya mdosi wao.

Inasemekana mdosi aliwapa makalameni hao kazi ya kuvuna mahindi na kuweka ghalani na siku ya kazi wakafika shambani tayari kuichangamkia.

Mambo yalienda kombo vibarua walipojua walikuwa wakipigwa darubini na kijana mmoja na wakateta kuwa mwajiri hakuwaamini.

“Mbona unakuja kazini ukiwa umeng’ara hivyo? Ama una nia gani hapa?” polo mmoja alimhoji barobaro naye akajibu kuwa kazi yake ilikuwa ya mnyapara wao.

Mara moja , hamaki zilipanda vibarua na wakaondoka shambani wakisema hawangevumilia kushukiwa kuwa wezi wa mahindi.