Dondoo

Demu kidomodomo apigwa kibuti

June 28th, 2019 1 min read

Na John Musyoki

ISIOLO MJINI

KIPUSA wa hapa alisutwa na majirani kwa kutaka kumtema mpenzi wake alipoamua kujiunga na chuo kuendelea na masomo.

Duru zinasema kwamba jamaa hakuwa amefanikiwa kujiunga na chuo kwa kukosa karo.

Juzi, jamaa huyo aliamua kuendeleza masomo yake baada ya kupata mfadhili wa kumlipia karo. Hata hivyo, mpenzi wake hakufurahishwa na uamuzi wa jamaa huyo na akamlaumu kwa kutaka kumtelekeza.

“Kwa hivyo umeamua kuniacha peke yangu hapa nyumbani. Uliniambia kwamba hukuwa na mpango wa kujiunga na chuo. Mimi sitaki mambo yako. Huu ndio wakati wa kufurahia maisha yangu nawe. Sasa utaenda kusoma nini na umezeeka,” demu alisikika akimwambia jamaa.

Inasemekana demu alitisha kumtema jamaa

“Kama utaniacha hapa ni heri tuachane kabisa. Siwezi kuvumilia maisha ya upweke,” demu alifoka.

Majirani walipandwa na mori waliposikia vitisho vya mwanadada huyo na wakamkashifu vikali.

“Wewe ni mwanamke sampuli gani, hata huna adabu. Kwa nini unampa mume wako presha? Kama njama yako ni kuponda raha potelea mbali. Sisi ni majirani wa mume wako na tutamtetea kufa kupona,” jirani mmoja alisikika akimponda demu.

Licha ya demu kutisha kumwacha mpenzi wake, jamaa alisimama kidete.

“Kama haja yako ni kuponda raha sina wakati wa kupoteza. Nimekuwa na ndoto ya kuendelea na masomo na wewe hutakuwa kizuizi cha mafanikio yangu.

“Umeniudhi sana na ukitaka ondoka. Nitakapomaliza masomo yangu nitatafuta mwanamke mwingine wa kuoa. Kwa sasa huna maana kwangu,” jamaa alisikika akimwambia mpenzi wake.

Demu hakuwa na jingine ila kufunganya virago vyake na kuondoka na jamaa akajiunga na chuo kuendeleza masomo yake bila bughudha.