Dondoo

Demu mlevi atimua wazazi

November 25th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

MBITINI, MACHAKOS

KIZAAZAA kilizuka mtaani demu alipowatimua wazazi wake, walipomtembelea nyumbani na kumpata amelewa chakari.

Inasemekana wazazi walikuwa wameenda kumjulia hali binti yao, na vile vile kumpa ushauri nasaha aachane na uraibu wake wa kupenda chupa.

Duru zinasema tabia hiyo ya ulevi imemletea nuksi mwanadada huyo na kumfanya avurugane na mume wake, ambaye aliamua kumuacha. Hata hivyo, wazazi wa kidosho hawakuamini walichokiona walipowasili katika makazi ya msichana wao.

“Walimpata akiwa amelewa kupindukia hata hajielewi. Isitoshe, alikuwa amechakaa sana!” alisimulia mdokezi wetu.

Alipowaona, demu aliwageukia na kuzua fujo huku akiwafokea baba na mamake kwa kumtembelea bila idhini.

“Mnataka nini hapa kwangu na sijawaalika. Hata sitawapatia viti vya kukaa wala chakula. Naomba muangalie penye mlango wa nyumba upo na muondoke sasa hivi,” demu alichemka.Wazazi wa demu walipigwa na butwaa wasiamini walichosikia.

Lakini ilibidi wasalimu amri binti yao alipogeuka simba akitisha kuwararua kwa viboko.

Kulingana na mdokezi, demu alinyayua fimbo alipoona wazazi wakisita kuondoka, na kuwatimua mbio huku akiwarushia cheche za maneno.

“Msiwahi kutia miguu yenu hapa kwangu. Hapa ni kwangu na sitaki ushauri wa mtu yeyote. Nitafanya ninavyotaka na mtu akileta kisirani atakiona cha mtema kuni,” kipusa alifoka.Inasemeka majirani waliwasaidia wazazi hao kuhepa ghadhabu za mwanadada, huku baadhi wakisema huenda kidosho huyo alikuwa akivuta vitu vingine kando na kuwa mlevi kupindukia.

Hata hivyo, baada ya muda yasemekana wazazi hao walisema hawatachoka hadi wamsaidie binti yao abadilike.

Walisema watahakikisha kuwa amepata ushauri unaofaa kutoka kwa watalaamu ili aache kulewa na kuharibu maisha yake.

“Walisisitiza kwamba ilikuwa jukumu lao kama wazazi kumsaidia mwana wao, hususan baada ya ulevi kufanya atemewe na mumewe,” alieleza mdokezi.