Dondoo

Demu mpenda chupa apoteza penzi

November 17th, 2019 1 min read

Na NICHOLAS CHERUIYOT

NYAGACHO, KERICHO

POLO wa mtaa huu aliaibika sana aliporudi nyumbani kutoka kibarua cha mjengo na kupata habari kwamba demu wake amelewa chakari na kulala nje ya baa.

Kulingana na mdokezi wetu, usuhuba wa wawili hawa ulianza kupitia mtandaoni ambapo jambo alimtupia mistari mifupi tu naye kipusa akameza chambo na kumuarifu kuwa angemtembelea wikendi.

“Jamaa alipandwa na mzuka kipusa alipoahidi kwamba atamuandalia asali arambe atakavyo, akiwasili nyumbani. Jamaa alishinda akipekua kurasa za Facebook kukodolea macho picha za mrembo, huku akiwaringia wenzake kuwa alikuwa gwiji katika uwanja wa mahaba,” mdaku alieleza.

Mambo yalienda shwari na wikendi ilipofika, demu alitimiza ahadi akafika kwa polo. Jamaa alikuwa akimsubiri kwa hamu na ghamu, damu ikimchemka kwa tamaa.

“Demu alikesha kwa jamaa na asubuhi ilipofika, jombi alimuacha chumbani akaelekea kazi ya mjengo. Alimpa demu hela ili asikose chochote siku hiyo,” mdokezi alieleza.

Jamaa aliporudi jioni alikuta chumba chake kikiwa wazi, akaingiwa na wasiwasi kwamba huenda demu amempora na kuingia mtini. Lakini alipoingia ndani alipata kila kitu shwari. Isitoshe, begi ya demu ilikuwa bado ndani.

Kaka alipouliza majirani aliko kipusa chake, alifahamishwa kwamba demu alionekana akielekea baa maarufu ya mji huu.

Pindi jamaa alipokea simu kutoka kwa rafiki yake akimtaka aende kumuokota demu wake mtaroni.

“Alipofika alimkuta kipusa akipayuka ovyo ovyo huku ameanguka kando ya mtaro wa maji taka,” mdokezi wetu alitueleza.

Jamaa alimbeba demu hadi kwake nyumbani. Siku iliyofuata alimuamsha kidosho asubuhi mapema na kumtaka afunganye virago aondoke. Vilevile, alimuonya kwamba hangetaka kumuona tena.