Dondoo

Demu ‘sumaku’ afukuzwa ploti

October 19th, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

HURUMA, NAIROBI

KIZAAZAA kilizuka katika ploti moja mtaani hapa, akina mama walipomkabili kidosho waliyedai alikuwa hatari kwa ndoa zao.

Duru zinasema kwamba walimpa mwanadada huyo makataa ya saa sita kuhama ploti walipomfumania mume wa mmoja wao katika nyumba yake.

Kisa hicho kilivutia si tu wapangaji wa ploti hiyo bali pia jirani waliofurika nje ya nyumba ya totoshoo huyo kushuhudia yaliyojiri.

“Hatuwezi kukuruhusu utupokonye waume zetu kutokana na tabia mbaya ya kuwaviringishia kiuno chako. Utahama utake usitake,” mama mmoja alipaza sauti.

Mama huyo alidai kuwa mumewe hakurejea usiku wa kuamkia siku hiyo na alipoamka alfajiri, alishtuka kumuona akitoka nyumba ya kidosho huyo.

“Leo ni leo. Ploti hii utaiona paa,” mama alitisha.

Wenzake walidai waume wengi katika ploti hiyo walikuwa wakimmezea mate kila wakati akitoka na kurejea katika chumba chake.

“Ahame! Ahame! Akachuuze mzinga wake kwingine, aache waume wetu,” mama mwingine aliunga mkono.

Walichemka kwa hamaki hivi kwamba hata juhudi za mhudumu wa ploti kuwatuliza hazikufaulu.

“Mna wivu, ndo maana mmeungana kunidhalilisha,” totoshoo alipiga kelele lakini hakuna aliyemsikiliza.

“Hakuna yeyote wa kukusikiliza hapa. Una bahati hatujakuzaba makofi. Hiyo tabia uliyo nayo, utaipeleka kwingine si hapa plotini,” mama mmoja alimwambia.

Duru ziliarifu kuwa wanawake hao walichukizwa na mitindo ya mavazi na kujipodoa ya mwanadada huyo

“Walidai alitumia sabuni maalum za kutunisha makalio na mikorogo ya kufifisha weusi wake wa asili ili apate shepu aliyotumia kuchota wanaume,” alieleza mdokezi. Kufikia adhuhuri ya siku hiyo, kidosho alikuwa amefunganya virago na kuondoka. Haijulikani alikohamia.