Shangazi Akujibu

Demu wangu aliniomba nauli akisema anatembelea wazazi lakini hajarudi

April 2nd, 2024 1 min read

Mpenzi wangu aliondoka wiki mbili zilizopita akaniambia anaenda kutembelea wazazi wake mashambani. Aliniomba pesa za nauli na bado mpaka sasa hajarudi. Inawezekana kuwa ameniacha?

Kama mpenzi wako alikuwa ameahidi kurudi na hajarudi licha ya kumpa nauli, ni lazima ana sababu zake. Labda ameamua kumaliza uhusiano wenu. Kama ana simu, mpigie umuulize.

Nataka kumuoa japo kuna mzigo wa watoto

Shikamoo shangazi. Mpenzi wangu ana watoto wawili aliyezaa na mshikaji wake wa awali. Nataka kumuoa lakini nahisi nitakuwa na mzigo mkubwa wa kulea kwa sababu ni lazima tuzae watoto wengine. Waonaje?

Ukimuoa mwanamke huyo watoto hao watakuwa wako na itabidi uwatunze sawa na wengine mtakaozaa. Usifumbwe macho na mapenzi ujitwike mzigo ambao unajua kwa hakika huwezi kubeba.

Imekuwa balaa kutema mmoja, nifanyeje?

Nimekuwa na wapenzi wawili na nimeanza kupoteza hisia kwa mmoja wao. Nataka kumuacha lakini naona vigumu kumwambia kwa sababu atahisi nilimtumia.

Huo wako ni ulaghai wa kimapenzi. Ukweli ni kuwa ataumia moyoni akijua una mwingine. Lakini itabidi umwambie badala ya kuendelea kumpotezea wakati.

Hatimizi wajibu wake kama mzee wa boma

Hujambo. Nilitengana na mume wangu miaka miwili iliyopita aliposhindwa kutimiza wajibu wake kwa familia. Bado nampenda na amekuwa akiniomba turudiane.

Ni wajibu wa mume kutunza familia yake. Ulimuacha mume wako kwa kushindwa kutekeleza wajibu huo. Kama anataka mrudiane, ni muhimu kwanza mshaurine na kuelewana kuhusu jambo hilo.