Shangazi Akujibu

Demu wangu anataka tupige picha pamoja tukiwa tuputupu, nishauri

May 13th, 2024 1 min read

Shikamoo, nimekuwa katika uhusiano na binti fulani chuoni na hata tunashiriki mahaba. Majuzi alianza kusisitiza tupigwe picha uchi tukiwa pamoja. Nina shauku kuhusu suala hili lakini pia sitaki kumkasirisha.

Marahaba! Yeye kutaka picha zenu za uchi inapaswa kukuogopesha. Hujui ni vipi zitatumika iwapo kwa bahati mbaya uhusiano wenu utakatika. Pili, zaweza kuishia kwa simu ya mtu mbaya kimakosa. Mwambie hutaki masihara na ikiwa anakupenda anafaa kuelewa aachane na mambo hayo.

Mke anapenda mahaba sana, hii ni kawaida?

Nimekuwa katika ndoa na mke wangu kwa miaka miwili sasa. Ameanza kunishinda nguvu kimahaba. Tunaporushana roho hatosheki kamwe huku nikijipata nimemaliza kabla yake. Hii ni kawaida?

Salama kaka. Miaka miwili ni michache sana kuchoshwa na mahaba. Itabidi uchangamke kutafuta jinsi ya kumridhisha mkeo la sivyo utajuta!

Kaka amenilipia hadi chuo lakini simtaki

Shangazi, nimechumbiana na jamaa kwa miaka mitano sasa. Alinilipia hata chuo kikuu, nakaribia kukamilisha masomo. Nimeanza kuhisi hanifai sababu hajafikia kiwango changu cha masomo. Nataka kumtema.

Fikra zako ni hatari sana na huenda zikasababisha maafa. Je, mbona ulikubali akulipie chuo kikuu ukijua wazi nia yake ni mwishowe akuoe, kisha sasa umekengeuka?

Mke wangu amekuwa katili wa kunipiga vita

Nampenda mke wangu sana. Tumeoana kwa miaka mitatu sasa. Tatizo ni kwamba tangu mwanzo wa ndoa yetu amekuwa akinichapa kila akikasirika. Naona aibu kuambia jamaa na marafiki masaibu yangu. Naomba usaidizi.

Hiyo ni dhuluma na sharti suala hili liangaziwe. Huenda wakati mmoja akakuumiza. Iwapo huna mtu mmoja tu unayeamini kumuambia, kuna nambari maalum unaweza kupiga kwa siri ili kuripoti dhuluma na utaelekezwa pahali pa kupata usaidizi. Usikimye.