HabariSiasa

DENI: Huenda Kenya ikapokonywa Bandari ya Mombasa na Uchina

December 20th, 2018 2 min read

NA BENSON MATHEKA

KENYA imo hatarini kupokonywa bandari ya Mombasa na serikali ya Uchina ili kulipia sehemu ya deni kubwa ambalo serikali inadaiwa na nchi hiyo, Mhasibu Mkuu wa serikali ameonya.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu inasema kwamba, China inaweza kutwaa bandari ya Mombasa serikali ikishindwa kulipa deni ililokopa kufadhili ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Sehemu ya kwanza ya reli hiyo kutoka Mombasa hadi Nairobi imekamilika kwa gharama ya Sh327 bilioni na ujenzi wa sehemu ya pili kutoka Nairobi hadi Naivasha unaendelea kwa gharama ya Sh150bilioni.

Ripoti za Shirika la Taifa la Takwimu (KNIBS), zinaonyesha kwamba, kwa jumula China ilikuwa ikidai Kenya zaidi ya Sh722 bilioni kufikia Juni mwaka jana.

Kwenye ripoti ya ukaguzi, iligunduliwa kuwa bandari hiyo ilitumiwa kama dhamana kuchukua mkopo wa kujenga reli ya kisasa na kwamba, shirika la reli la Kenya (KRC) likishindwa kutimiza jukumu lake, bandari inaweza kutwaliwa na China.

Kulingana na ripoti hiyo, mapato kutoka bandari hiyo muhimu inayosimamiwa na Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) yatatumiwa kulipa mkopo ambao serikali ilichukua kutoka China EXIM Bank kujenga reli ya kisasa iwapo Kenya itashindwa kulipa.

Kuna wasiwasi kuwa mapato kutoka kwa huduma za reli hiyo hayatoshi kulipa mkopo huo huku Sh1 bilioni zilizopatikana mwaka mmoja baada ya kuzinduliwa zikitumiwa kugharimia ukarabati. Kwa siku, SGR hupata Sh2.7 milioni na kashfa ya wizi wa pesa pia imeripotiwa huku raia watatu wa China wakishtakiwa kwa wizi wa mamilioni ya pesa.

Kinachoweka bandari hiyo kwenye hatari ya kutwaliwa na China, ni ufichuzi kuwa Kenya haikukinga mali yake kwenye mkataba wa mkopo huo.

Ripoti inasema kwamba, Kenya iliondoa kinga kwa mali ya KPA ilipotia sahihi makubaliano ya kupata mkopo huo. Ripoti inasema KPA haikufichua kwamba bandari ilitumiwa kama dhamana ya mkopo.

“Kesi yoyote dhidi ya mkopeshaji haitakuwa na kinga yoyote kwa sababu serikali iliondoa kinga za mali ya KPA kwa kukubali kutia sahihi mkataba huo na kuweka mali ya KPA kwenye hatari,” inaeleza ripoti hiyo.

Inasema kwamba, mzozo wowote kuhusu ulipaji wa mkopo huo hauwezi kutatuliwa Kenya.

“Mkataba huo unabagua kwa sababu iwapo kutazuka mzozo na China Exim Bank kwa kushindwa kulipa, juhudi zozote za upatanishi zitapelekwa China ambayo haki haitahakikishwa katika kuutatua,” inaeleza ripoti iliyotayarishwa na F T Kimani kwa niaba ya Mkaguzi Mkuu Dkt Edward Ouko.

Takwimu za KPA zilionyesha kuwa, mapato yake yaliongezeka kwa Sh3,132,843,00 hadi Sh42,736,520,000 kutoka Sh39,603,677,00 kufikia Juni 30, 2017.

Hii ni ripoti ya pili mwaka huu kuonyesha kuwa kuna hatari ya mali ya Kenya kutwaliwa na China kufuatia mlima wa madeni.

Mnamo Novemba, shirika la kimataifa la Moody’s linalofuatilia na kutathamini madeni lilionya kuwa China inaweza kutwaa bandari ya Mombasa.

Nchi hiyo tayari imetwaa mali ya serikali ya Zambia iliposhindwa kulipa deni na kwa sasa inasimamia Shirika la Habari la nchi hiyo ili kujilipa deni hilo.