HabariSiasa

DENI: Kenya Power, KQ, KPA, KenGen, KBC na KR hatarini kupigwa mnada

April 26th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

HUKU serikali ikiendelea kuomba mikopo zaidi nchini China, mashirika yake manane makuuu yako katika hatari ya kupigwa mnada kuwa kushindwai kulipa jumla ya Sh147.7 bilioni ambazo ilikuwa imekopa kutoka nje kufikia Desemba, 2018.

Kulingana na ripoti ya Idara ya Utayarishaji wa Bajeti Bungeni (PBO) iliyowasilishwa Alhamisi kwa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, mashirika ambayo mali yao yako katika hatari ya kuuzwa ni; Kampuni ya Kusambaza Umeme Nchini (Kenya Power) inayodaiwa Sh14.02 bilioni, Shirika la Ndege Nchini (KQ) 76.39 bilioni, Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA) Sh33.7 bilioni, Kampuni ya Kuzalisha Umeme Nchini (KenGen) Sh10.86 bilioni. Shirika la Utangazaji Nchini (KBC) Sh6.95 bilioni.

Mashirika mengine yanayodaiwa ni; Shirika la Reli Nchini (KR) Sh4.59 bilioni, Halmashauri ya Ustawi wa Mito ya Tana na Athi (TARDA) Sh542 milioni na Kampuni ya kutengeneza Saruji, East African Portland Cement Sh674 milioni.

Ripoti hiyo inasema mali ya mashirika hayo yalitumiwa na serikali kama dhamana kwa mikopo iliyopata kutoka kwa China na Kitengo cha kufadhili maendeleo kimataifa katika Benki ya Dunia (WB).

Katika ripoti yake iliyowasilisha bungeni mapema mwaka huu, Wizara ya Fedha ilisema deni la Kenya linakisiwa kufikia Sh5.6 trilioni itimiapo Juni mwaka huu. Na mzigo huo wa deni unatarajiwa kupanda hadi Sh7 trilioni ifikapo 2022 Rais Uhuru Kenyatta atakapokuwa akiondoka mamlakani baada ya kukamilisha kipindi chake cha pili na cha mwisho.

Rais Uhuru Kenyatta yuko nchini China ambako anahudhuria kongamano kuhusu ujenzi wa miundomsingi kati ya China na Afrika, ambapo alifanya kikao na Rais wa nchi hiyo Xi Jinping kuhusu masuala kadhaa.

Japo hakutangaza, Rais pamoja na Jinping walikuwa wakitarajiwa kutia sahihi mkopo wa Sh368 bilioni ambao Kenya ilienda kukopa China, kukamilisha ujenzi wa reli ya SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, ambaye pia yuko China, Jumamosi wiki iliyopita alitangaza kuwa wangeandamana na Rais katika ziara hiyo ya kukopa.

Mkopo huo unamzidishia Mkenya mzigo zaidi kiuchumi, wakati Kenya kwa sasa ina zaidi ya deni la Sh5 trilioni.

Utafiti wa shirika la Masuala ya Kiuchumi (IEA) Jumatano ulionyesha kuwa hadi Septemba mwaka jana, kila Mkenya alikuwa akidaiwa Sh108,500 za madeni ambayo serikali imekopa. Hii ni ikilinganishwa na Sh180,839 ambazo ndizo jumla ya mapato ya nchi (GDP), kulingana na jinsi uchumi ulikuwa mwaka jana.

Utawala wa Rais Kenyatta umekuwa na kiu ya kukopa pesa, rekodi zikionyesha kuwa tangu alipoingia uongozini mnamo 2013, madeni ya taifa yamekuwa yakipanda, hali ambayo inazidi kufanya hali ya maisha kuwa ngumu kwa Wakenya wa kawaida.

Ripoti ya utafiti wa IEA ilionyesha kuwa tangu 2014, kiwango cha pesa ambazo Kenya inatumia kulipa riba za mikopo kimekuwa kikipanda kwa mabilioni ya pesa, lakini serikali inazidi kuendelea mikopo.

Tangu 2013, kiwango hicho kimepanda kutoka Sh331 bilioni, hadi Sh870 bilioni mwaka jana, ambazo serikali inatumia kugharamia riba za mikopo pekee, kabla haijalipa mikopo yenyewe.

Katika miaka ya 2015, 2016 na 2017 kiwango hicho kilipanda kwa viwango vya Sh417 bilioni, Sh466 bilioni na Sh649 bilioni mtawalia.

Shirika la IEA aidha lilikosoa Kenya kwa kupenda kukopakopa kutoka China ambayo ina riba za juu na inayotoa muda mfupi kwa madeni yake kulipwa, bila kufuatilia ikiwa pesa inazokopesha zinatumiwa ifaavyo.

Kati ya mataifa ambayo Kenya imekuwa ikikopa, China inaongoza kwa asilimia 70 ya madeni, ikifuatiwa na Japan kwa asilimia 11 na Ufaransa kwa asilimia saba.

“Mikopo kutoka China ni ya benki ya kibiashara ambayo inatoza riba ya juu na inayohitaji muda mfupi kulipia, ikilinganishwa na ile ya kutoka mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia,” akasema John Mutua, afisa wa utafiti IEA.