Habari Mseto

Densi yachangamsha katika tamasha za muziki

August 6th, 2019 1 min read

Na ANTHONY NJAGI

WANAFUNZI wa shule ya Bridge Mitume Academy kutoka Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia walitia fora jana waliposakata densi ya kiasili ya jamii ya Wabukusu katika Tamasha za Kitaifa za Muziki zinazoendelea katika Chuo Kikuu cha Kabarak.

Densi hiyo inayofahamika kama ‘Kamabeka’ iliwaacha wengi wakiwa na hamu ya kutaka kuendelea kutazama miondoko zaidi.

Densi hiyo huchezwa na wanaume na wanawake kusherehekea mambo mema.

Mtindo ambao kikosi hicho kilitumia kujitosa jukwaani pia uliteka nyara nyoyo za wengi.

Waamuzi waliridhishwa na densi ya wanafunzi hao hivyo kuwatawaza washindi.

Baada ya kutumbuiza jukwaani na kushinda tuzo, wanafunzi hao walienda nje ya ukumbi na kuendelea kusakata densi huku wakizunguka kote chuoni Kabarak.

Mwalimu wa muziki wa shule hiyo, John Ambeyi alitaka densi ya wanafunzi wake irekodiwe ili isije ikasahaulika baada ya siku chache.

“Kuna haja nyimbo zinazochezwa hapa zirekodiwe na watengenezaji wa filamu wazitumie kama njia mojawapo ya kuhifadhi utamaduni wetu na kuzipatia shule husika mapato,” akasema.

Mbali na densi za jamii ya Kiluhya, kitengo kingine kilichofana ni densi za jamii ya Mijikenda.

Katika kitengo hiki, wanafunzi kutoka Shule ya Msingi ya Consolata, Harambee Gardens, Yala Township, Lenana, Makutano AIC na Shimo La Tewa Borstal zilionyeshana ubabe wa kusakata densi za kiasili.

Mashindano hayo yaliyoanza wikendi iliyopita yamevutia washiriki kutoka kila pembe ya nchi.