Michezo

Depay ajiengua Lyon akitarajiwa kuzinduliwa Barcelona

October 5th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

FOWADI raia wa Uholanzi, Memphis Depay, 26, amekubali kusajiliwa na Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), vyanzo kadhaa vimesema.

Kwa mujibu wa Juninho Pernambucano ambaye ni mkurugenzi wa soka kambini mwa Olympique Lyon, Ufaransa, Depay aliachwa nje ya kikosi kilichoambulia sare ya 1-1 na Olympique Marseille mnamo Oktoba 4, 2020 ili akamilishe uhamisho wake hadi Barcelona.

“Nyota huyo wa zamani wa Manchester United hatakuwa sehemu ya kikosi chetu muhula huu. Amejiunga na Barcelona,” akasema Juninho.

Mchezaji mwingine anayetazamiwa kuingia katika sajili rasmi ya Barcelona ni Eric Garcia ambaye tayari ameachiliwa na Manchester City.

Mkataba kati ya Garcia na Man-City ulitarajiwa kukatika rasmi mwishoni mwa msimu huu. Kuachiliwa kwake kulichochewa na hatua ya Man-City kumsajili beki raia wa Ureno, Ruben Dias aliyeagana na Benfica ya Ureno kwa kima cha Sh9.1 bilioni mnamo Septemba 29, 2020.

Hadi kuondoka kwake kambini mwa Lyon, Depay alikuwa amefungia kikosi hicho jumla ya mabao 58 kutokana na mechi 144 tangu ajiunge rasmi na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ufaransa kutoka Man-United mnamo 2017.

Depay alishindwa kutamba katika EPL kwa miaka mitatu. Sogora huyo aliyesajiliwa na kocha Louis van Gaal kwa kima cha Sh4.3 bilioni mnamo 2015, alifunga mabao saba pekee kutokana na mechi 53.

Ataungana sasa na Mholanzi mwenzake Ronald Koeman, ambaye alipokezwa mikoba ya Barcelona mwanzoni mwa msimu huu baada ya miamba hao wa Uhispania kuagana na mkufunzi Quique Setien.