Dereva afungwa maisha kwa kusaidia magaidi kuteka Wacuba

Dereva afungwa maisha kwa kusaidia magaidi kuteka Wacuba

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA dereva kaunti ya Mandera aliyewasaidia magaidi wa Al Shabaab kuwateka nyara madaktari wawiili kutoka Cuba miaka mitatu iliyopita jana alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Issack Ibrein Robow, 42 alisukumiwa kifungo hicho na hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Nairobi Bi Martha Nanzushi. Akimuhukumu Robow, Bi Nanzushi alisema kitendo hicho cha Robow aliyekuwa dereva wa Dkt Assel Herrera Correa na Dkt Landy Rodriguez Hernandez kilitishia kuzorotesha uhusiano wa Kenya na Cuba ambayo ilikuwa imefadhili madaktari kutoa huduma za afya nchini Kenya.

Baada ya kuzuiliwa mahala pasipo julikana kwa mwaka mmoja madaktari hao wawili waliachiliwa na kurudi kwao Cuba Akasema Bi Nanzushi,“Madaktari hao wataishi na woga na kovu la kutekwa nyara maisha yao yote na magaidi wa Al Shabaab. Robow alifanya uhalifu mkubwa unaofaa aadibiwe vikali.”

Mbali na kutekeleza kitendo cha ugaidi Robow alihukumiwa kifungo cha miaka 50 kwa kuteka nyara madaktari hao na kuwasaidia magaidi wa Al Shabaab kuwateka nyara Dkt Correa na Dkt Hernandez.

Wakati wa kutekwa nyara kwa madaktari hao Konstebo Katambo aliuawa kinyama. Robow alikuwa akiendesha gari la Serikali nambari ya usajili GKA 221U, Toyota Hilux. Kwa makosa ya kuteka nyara alifungwa miaka 25 na kuwasaidia magaidi wa Al Shabaab kuwateka nyara madaktari hao na kuuawa kwa Konstebo Katambo mshtakiwa alifungwa miaka 25.

Hakimu mwandamizi aliyemfunga maisha dereva wa kaunti ya Mandera kwa utekaji nyara wa madaktari wawili wa Cuba…Picha/RICHAED MUNGUTI

Vifungo hivyo vitatumika wakati mmoja. Mahakama ilisema Katambo alipoaga mkewe alikuwa mja mzito na “sasa mwanawe yuko na umri wa miaka mitatu.Mtoto huyo hajui uzuri wa baba na hatawahi kutokana na ukora wa Robow.”

Hakimu alisema dereva huyo alikosea nchi hii heshima kwa kuwasaidia magaidi kutekeleza uhalifu unaokemewa kote ulimwenguni. “Mwenzake Mutundo Kitambo aliyeponea shambulizi hilo alisema anaishi kwa uchungu mwingi aliposhuhudia”

“Kitendo hicho cha ugaidi kilifanya hospitali ya kaunti ya Mandera kutopelekewa madaktari kufikia sasa. Wananchi wameumia kutokana na kitendo hiki cha kinyama.Magaidi hao walitia mchanga uhusiano wa Kenya na Cuba kudorora,” alisema Bi Nanzushi.

Hakimu aliyechukulia hilo kuwa kosa la kwanza alisema “mahakama inahusudu ugaidi na haitasita kuadhibu kwa nguvu zake zote magaidi.” “Kwa kosa la kwanza la kuwasaidia magaidi wa Al Shabaab kuwateka nyara madaktari hao raia wa Cuba utatumikia kifungo cha maisha,” alisema Bi Nanzushi.

Mahakama ilimwadhibu kutumikia tena kifungo cha miezi sita kwa kujipatia kitambulisho cha kenya kinyume cha sheria mnamo Julai 6,2000. Bi Nanzushi aliagiza atumikie miezi hiyo sita akikamilisha kifungo hicho.

Wakili Chacha Mwita aliyemtetea mshtakiwa aliomba afungwe kifungo cha nje akisema yuko na majukumu mengi ikitiliwa maanani ni baba wa watoto 11 wanaomtegemea. Mwita aliomba mahakama isikize ombi la kurejeshewa kitambulisho mshtakiwa aliyesema aliachiliwa kwa shtaka aliyodaiwa ni raia wa Somalia.

Kiongozi wa mashtaka Harrison Kiarie alieleza mahakama idara ya usajili wa watu imeanza utarartibu wa kuharibu kitambulisho hicho. Bi Nanzushi alisema hawezi kujiingiza katika suala la kitambulisho kwa vile amepitisha hukumu na hawezi kufungua tena suala la kitambulisho hilo.

“Sasa sihusiki na kesi hii tena. Mshtakiwa amehukumiwa.Peleka ombi hilo mahakama kuu,” Bi Nanzushi alimweleza Mwita.

Hakimu mwandamizi aliyemfunga maisha dereva wa kaunti ya Mandera kwa utekaji nyara wa madaktari wawili wa Cuba…Picha/RICHARD MUNGUTI

You can share this post!

Wanasiasa wanawake kufundishwa kujikinga na dhuluma...

Waziri adai wakuu wa shule husajili watahiniwa hewa...

T L