Kimataifa

Dereva ashtuka kupata joka la futi 12 ndani ya gari

June 5th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA na VALENTINE OBARA

BANGKOK, THAILAND

DEREVA aliyekuwa akitatizika kuendesha gari lake alipigwa na butwaa alipopata kulikuwa na joka la futi 12 ndani ya boneti.

Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha joka likiwa kwenye gari ya dereva huyo aliyetambuliwa kama Tee Natwijit.

Iliripotiwa kuwa jamaa huyo aliyesemekana kuwa mwenye duka, hakujua kulikuwa na joka ndani ya gari lake hadi wateja walipomwambia wameona mkia ukining’inia kutoka kwa gari lake.

Wakati alipoenda kufungua boneti, alikutana ana kwa ana na joka la kutisha ambalo ilibainika lilikuwa na uzani wa kilo 30.

“Ilibidi afunge boneti kwa haraka kisha akaita maafisa wa kutunza wanyama ambao walikuja wakaondoa joka hilo lililokuwa limejikunja kwenye injini,” mashirika ya habari yakasema, na kuongeza kuwa mnyama huyo alirudishwa kichakani.

Kwenye mahojiano na vyombo vya habari, Bw Natwijit alinukuliwa kusema anashuku joka hilo ndilo lilikuwa likila kuku wake nyumbani ambao wamekuwa wakitoweka kwa njia za kustaajabisha.

Afisa mmoja aliyehusika katika shughuli ya kuondoka joka hilo alisema ni kawaida nyoka kutafuta mahali pa kujisitiri ambako kuna joto na ukavu wakati wa msimu wa mvua.

“Injini ya gari ni mandhari shwari sana kwa minajili hii. Inafaa watu wawe wakikagua magari yao kabla waanze kuendesha gari,” akasema afisa huyo.