Na GEOFFREY ANENE
MADEREVA 16 wamethibitisha kushiriki raundi ya kwanza ya Mbio za Magari za Kitaifa nchini Kenya (KNRC) hapo Februari 5 katika kaunti ya Machakos.
Dereva Karan Patel anaongoza orodha hiyo na atatoka jukwaani wa kwanza katika bustani ya Machakos People’s Park saa mbili asubuhi.
Karan anaelekezwa na Tauseef Khan katika gari la Ford Fiesta. Atakuwa akitetea taji alilonyakua mwaka jana alipomaliza katika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Hamza Anwar anayeshiriki Mbio za Magari za Dunia za chipukizi (JWRC) mwaka huu, na Jasmeet Chana katika nafasi tatu za kwanza.
Jasmeet atakuwa wa pili kutoka jukwaani akishirikiana na Ravi Chana katika Mitsubishi EVO10. Aakif Virani/Azhar Bhatti (Skoda Fabia), Eric Bengi/Waigwa Murage (Mitsubishi EVO10) na Evans Kavisi/Absalom Aswani (Mitsubishi EVO10) watafunga nafasi tano za kwanza kutoka jukwaani katika mbio hizo za kilomita 154.82 zitakazofanyika katika shamba la Lisa Farm.
Bingwa wa Mbio za Afrika kitengo cha chipukizi mwaka 2021 McRae Kimathi aliyeshiriki JWRC mwaka 2022, ataanza katika nafasi ya saba akishirikiana na Mwangi Kioni, nyuma ya mwenzake Jeremiah Wahome anayeelekezwa na Victor Okundi. Watapaisha magari ya Ford Fiesta.
Karan aliibuka bingwa wa taifa 2022 baada ya kutawala raundi ya Kajiado, Nakuru, Equator, Eldoret, Nanyuki, Machakos na Guru Nanak, akikosa kumaliza Bamba Rally Mombasa kwa sababu ya hitilafu ya giaboksi.