Na GEOFFREY ANENE
BINGWA mara tano wa Mbio za Magari za Kitaifa nchini (KNRC) kitengo cha magari ya 2WD, Leonardo Varese ana imani tele ya kufunga mwaka 2021 vyema wakati wa KCB Guru Nanak Rally.
Dereva huyo mkazi wa Nairobi alirejea katika mbio za magari baada ya miaka miwili wakati wa duru ya saba (Nanyuki Rally) mnamo Oktoba 9 alipokamata nafasi ya 15.Varese, ambaye atashirikiana na mwelekezi wake Kigo Kareithi katika gari la Toyota Auris 2WD, amefichua kuwa lengo lake la kwanza wikendi hii ni kukamilisha mbio hizo za kilomita 154 zitakazoandaliwa na klabu ya Sikh Union Nairobi barabara katili za Il-Bissel kaunti ya Kajiado.
Dereva huyo anayedhaminiwa na kampuni ya kamari ya Sportpesa pia atatumia Guru Nanak kujiandaa kushiriki duru zote tisa msimu ujao.“Guru Nanak Rally ni mojawapo ya duru ninazopenda sana kwenye kalenda ya KNRC. Hata hivyo, tumepata ushindi mmoja pekee katika duru hiyo, mwaka 2009,” alisema Varese hapo jana. “Maandalizi ya Guru Nanak yamepamba moto. Tulianza matayarisho baada tu ya Nanyuki,” alifichua.