Habari Mseto

Dereva wa Kenya afariki mpakani Uganda akisubiri ukaguzi

June 15th, 2020 1 min read

NA DAILY MONITOR

Polisi na maafisa wa afya nchini Uganda Wilaya ya Busia wanafanya uchunguzi kuhusiana na kifo cha dereva wa lori wa Kenya aliyepatikana amefariki Uganda.

Mwili wa Bw Samuel Kinyua Wangware mwenye miaka 35 na mkazi wa Mathira kaunti ya Nyeri, Kenya ulipatikana na mwenzake Bw Paul Njoronge Jumamosi ndani ya lori alilokuwa akiendesha katika kituo cha ukaguzi cha Busitema Wilaya ya Busia.

Kamanda wa polisi  wa Wilaya ya Busia alisema kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini kilichosababisha kifo hicho.

Bw Njoroge alisema kwamba alikuwa amesimamisha lori lake ili kusalimia mwenzake kwa ghafla akapata amefariki.

“Nilikuwa naelekea kwenye mpaka wa Malaba, nikaona lori lake nikasimama kumsalimia kwa bahati mbaya nikapata amefariki,” alisema Bw Njoroge.

Duru za kuaminika zilisema kwamba dereva huyo alionekana ameegesha lori lake lenye nambari ya usajili KAT578T, katika kituo cha ukaguzi cha Busitema akielekea Nairobi kutoka Kampala  na alisikika akisema kwamba alikuwa mgonjwa.

Alionekana pia akibadilisha tairi.