Habari Mseto

Dereva wa teksi ashtakiwa kumbaka mteja na kuiba mali yake

December 3rd, 2019 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

DEREVA wa magari ya teksi anayedaiwa alimbaka mteja wake na hatimaye kumwibia simu ya mkononi yenye thamani ya Sh35,000 atakaa ndani kwa siku 18 polisi wakamilishe uchunguzi.

Shem Mogaka Nyakundi anayedaiwa alimbaka mlalamishi siku 10 zilizopita alifikishwa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani Bi Muthoni Nzibe.

Mbele ya Bi Nzibe, Nyakundi, alikanusha mashtaka mawili ya wizi wa simu muundo wa Techno na kupatikana na mali ya wizi katika mtaa wa Tassia ulioko Embakasi kaunti ya Nairobi mnamo Novemba 22, 2019.

Mshtakiwa kupitia kwa wakili wake aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na afisa anayechunguza kesi hiyo Inspekta Eunice Njue aliyeambia mahakama kwamba “mbali na kesi hii ya wizi pia tunaendelea na uchunguzi wa ubakaji dhidi ya mshtakiwa.”

Insp Njue alisema mshtakiwa anadaiwa alimbaka mteja wake kwa siku nzima kisha “akamlazimisha kuoga ndipo aharibu ushahidi.”

Mahakama ilielezwa mshtakiwa alikodiwa na mlalamishi kumpeleka Ruiru kutoka eneo la Lang’ata.

“Badala ya kumpeleka mlalamishi Ruiru mshtakiwa alimpeleka kwa nyumba yake mtaani Tassia , Embakasi Nairobi na kumzuilia kwa nyumba siku nzima,” alisema Inspekta Njue.

Mahakama ilielezwa mshtakiwa alipotoka pale hakujua aliko kwa vile alikuwa hana ufahamu.

Hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe alisema mlalamishi alipeleka ripoti ya kubakwa kwake katika kituo cha polisi cha Ruiru.

“Katika kituo cha Ruiru mlalamishi alishauriwa awasilishe ripoti hiyo ya kubakwa katika kituo cha polisi cha Embakasi,” alisema Insp Njue.

Mahakama ilielezwa kabla ya ripoti nyingine kupelekwa kituo cha Polisi cha Embakasi mlalamishi alienda hospitali ya Nairobi Womens Hospital kupimwa na kupewa dawa za kuzuia maradhi hatari kumpata.

“Bado sijapata fomu iliyotiwa sahihi na Daktari aliyemtibu mlalamishi,” alisema

Mahakama ilielezwa Daktari huyo atarudi kazini Ijumaa wiki hii.

“Shtaka kuu dhidi ya mshtakiwa ni ubakaji na wala sio wizi wa simu,” Insp Njue alimweleza hakimu.

Alisema kuwa mashtaka mengine yatawasilishwa dhidi ya mshtakiwa uchunguzi wa ubakaji ukikamilishwa.

Wakili anayemtetea mshtakiwa alipinga ombi la kumnyima mshtakiwa kwa dhamana akisema, “dhamana ni haki ya kila mshukiwa.”

Aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana na kumwakikishia hakimu kwamba mshtakiwa atarudi mahakamani kuendelea na kesi itakapoanza kusikizwa.

Hakimu aliamuru mshtakiwa azuiliwe hadi Desemba 19, 2019 korti itakapoamua iwapo ataachiliwa kwa dhamana au la.

Shtaka la wizi lilisema mnamo Novemba 22, 2019 katika mtaa wa Tassia aliiba simu yenye thamani ya Sh35,000.

Pia alishtakiwa kupatikana na mali aliyojua imeibiwa ama kupatikana kwa njia isiyohalali.