Habari Mseto

Dereva wa teksi ashtakiwa kupora mteja wa kike na kumdhulumu kimapenzi


DEREVA wa teksi ameshtakiwa kumdhulumu kimapenzi mteja wake mwanamke na kumnyang’anya kimabavu pesa na simu kisha akamfurusha nje ya gari mtaani Eastleigh Nairobi miezi tisa iliyopita.

Hassan Abdikadir Sharif aliyeshtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi alikana mashtaka mawili dhidi yake.

Sharif aliyeagizwa azuiliwe rumande hadi Juni 26, 2024 atakapopelekwa katika mahakama ya Makadara alikuwa ametoroka tangu 2023.

Sharif alikuwa ameshtakiwa katika mahakama ya Makadara.

Alifikishwa katika mahakama ya Milimani kufuatia agizo la Jaji Mkuu Martha Koome kwamba kesi zote za Makadara zitajwe mbele ya mahakama ya Milimani kufuatia kufungwa kwa korti hiyo.

Mahakama ya Makadara ilifungwa Juni 13, 2024 baada ya hakimu mkazi Monica Kivuti kupigwa risasi na kuuawa na afisa wa polisi Inspekta Samson Kipchirchir Kipruto.

Insp Kipruto aliuawa papo hapo na afisa mwingine wa polisi.

Wakati wa kisa hicho, maafisa watatu wa polisi walijeruhiwa.

Mahakama ilifungwa kuimarisha usalama kisha kesi zote zikaagizwa zitajwe mahakama ya Milimani.

Alipofikishwa mbele ya Bw Ekhubi Sharif alikana kumnyang’anya abiria wake mwanamke aliyetambuliwa kwa jina RMS mkoba wa bei ya Sh1,500, simu ya kiunga mbali ya thamani ya Sh150,000 na pesa tasilimu Sh30,000.

Sharif aliomba aachiliwe kwa dhamana kisha kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki akapinga akisema “mshtakiwa huyu alitoroka miezi tisa iliyopita.”

Bi Kariuki alifichua mshtakiwa alikamatwa na maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) baada ya kutoroka na kuzuliwa hadi Alhamisi aliposhtakiwa kwa makosa mawili ya wizi wa mabavu na dhuluma za kimapenzi.

“Maafisa wa DCI walimtia nguvuni mshtakiwa baada ya kutoroka miezi tisa,” Bi Kariuki alifichua.

Aliomba mahakama ikatae ombi la dhamana ya mshtakiwa.

“Naomba hii mahakama iamuru mshtakiwa arudishwe hadi makadara alikoshtakiwa mwaka uliopita kisha akataoroka akawasilishe upya ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana,” Bi Kariuki alisema.

Bi Kariuki alisema dhamana ya mshtakiwa ilikuwa imetwaliwa na serikali na anastahili kukaa rumande.

Mwaka uliopita Sharif alishtakiwa mbele ya mahakama ya Makadara kwa wizi lakini RMS akalalamika kwa DCI na DPP kuwa alidhulumiwa kimapenzi na kwamba mshtakiwa hakushtakiwa alivyostahili.

Shtaka la dhuluma za kimapenzi liliongezwa.

“Utakaa rumande hadi Juni 26, 2024 utakapofikishwa katika mahakama ya Makadara,” Bw Ekhubi alimweleza mshtakiwa.

Hakimu aliamuru mshtakiwa azuiliwe katika gereza la viwandani hadi wiki ijayo Juni 26, 2024.