Desai FC yabwaga Kitisuru Allstars huku Kibagare Slums ikitoka sare na Rosslyn FC

Desai FC yabwaga Kitisuru Allstars huku Kibagare Slums ikitoka sare na Rosslyn FC

NA PATRICK KILAVUKA

KULISHUHUDIWA matokeo mseto katika michuano ya Ligi ya Kaunti, FKF, Nairobi West ambayo iliandaliwa ugani Kihumbuini, Jumapili.

Desai FC waliibwaga Kitisuru Allstars 1-0 kupitia Kevin Yunah dakika ya saba.

Mchezaji wa Desai FC ajipata katika kabiliano kali dhidi ya wachezaji wa Kitisuru Allstars. PICHA | PATRICK KILAVUKA
Mchezaji Moses Ochieng wa Desai FC – jezi ya kijani kibichi – akikakiliana na John Muhanji wa Kitisuru Allstars. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Kangemi Patriots walijikuta kwenye kona mbaya pale ambapo walizabwa 4-1 na UoN Olympic, japo Patriots ndio walikuwa wa kwanza kufungua akaunti ya magoli kunako dakika ya pili kupitia Collins Vudulani, furahia hiyo haikudumu kwa muda kabla Olympic kuanza kujituma na bahati yao ikaanza kusimama kunako dakika ya sita ambapo Evans Maosa alipachika kimiani goli rahisi na kuacha difensi ya Patriots kinywa wazi kabla Kevin Kimutai kuzidisha ujanja na kufunga la pili dakika ya 26.

Aidha, kipindi pili kilianza kwa kasi sana lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda,Olympic walikuwa wanavizia lango la Patriots kama viwavi na kunako dakika ya 62, Isaac Ogola alicheka na nyavu la tatu kabla William Babayaro kukalifisha wapinzani kunako dakika ya 85 na kuzamisha chombo chao zaidi.

Katika mechi nyingine, Kibagare Slums ambayo inajitanua kujaribu bahati ya kunyakua taji la msimu huu, walibahati mithili ya mtende kuzoa alama kutoka kwa Rosslyn FC ambao walikuwa wamewakalia ngumu katika kipindi cha kwanza kwa kuwalazimishia sare tasa kabla kufunga goli la kusawazisha la dakika ya 50 kupitia Vincent Mujumba, japo Rosslyn ndio walitangulia kufuma baada ya mchezaji uyo huyo Mujumba kujifunga dakika ya 48.

  • Tags

You can share this post!

PSG watumia mabilioni ya pesa kushawishi Mbappe kuwaruka...

Salah na Son wagawana Kiatu cha Dhahabu baada ya kuibuka...

T L