Michezo

Deschamps aeleza hofu kuhusu kipa Areola

September 4th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

KOCHA wa Ufaransa Didier Deschamps ameeleza hofu yake kwamba fomu ya kipa wa timu ya taifa Alphonse Areola itadorora zaidi akikosa kuwajibishwa uwanjani baada ya kujiunga na vigogo wa soka nchini Uhispania, Real Madrid.

Areola amenyakia Ufaransa mara tatu na alikuwa kipa nambari tatu wa ‘Les Blues’ nyuma ya Hugo Lloris na Steve Mandanda, timu hiyo iliposhinda Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka wa 2018.

Alihamia Real Madrid siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho wa wachezaji.

Mnyakaji huyo mwenye umri wa miaka 26 pia amejumuishwa na Deschamps kwenye kikosi cha kufuzu kipute cha Euro 2020 ambacho kitawakutanisha na Albania na Andora kuanzia wikendi hii.

Ni kutokana na uzito wa mechi zinazonukia ambapo Deschamps, nyota wa zamani wa Ufaransa ameeleza wasiwasi wake kuhusu uwezekano finyu wa kipa huyo tegemeo kupata nafasi ya kutosha kushiriki mechi mbalimbali za Los Blancos hasa kwenye Ligi ya Uhispania(La Liga) na Klabu Bingwa Barani Uropa (Uefa).

“Tutaona baada ya muda iwapo maoni yangu ni kweli au la. Huwa ni vizuri kwa makipa kushirikishwa kwenye mechi nyingi iwezekanavyo. Hata hivyo, sioni kama Areola atamlisha benchi kipa tegemeo wa Real Madrid Thibaut Courtois, ni vigumu sana,” akasema Deschamps.

Kuwa vigumu

Kocha huyo alikiri kwamba itakuwa vigumu kumshirikisha kipa huyo kwenye mechi zijazo kwa sababu uwezekano wake wa kuchezea Real Madrid mechi nyingi ni finyu sana kutokana na weledi wa Courtois.

“Atakuwa nambari mbili na sijui kama atapata nafasi ya kucheza. Iwapo atakosa mechi kadhaa, itakuwa vigumu kumjumuisha kikosini hasa kwenye mechi za kimataifa zitakazonoga mwezi Oktoba,” akaongeza.

France itakuwa wenyeji wa Albania katika uga wa Stade de France Jumamosi kisha ikabane na Andorra mnamo Jumanne katika mechi za Kundi H za kufuzu Mataifa Bingwa Barani Ulaya(EURO 2020). Les Blues wanaongoza kundi hilo kwa alama tisa baada ya kujibwaga uwanjani mara nne.

Areola ambaye ametajwa kwenye kikosi cha kushiriki michuano hiyo miwili atakuwa akiwania kuchezeshwa langoni dhidi ya nyani wa Tottenham Hotspur Hugo Lloris na mwenzake wa Lille Mike Maignan.