Desturi ya aina yake kisiwani Lamu inayozipatia mashua ‘uhai’ baharini

Desturi ya aina yake kisiwani Lamu inayozipatia mashua ‘uhai’ baharini

Na KALUME KAZUNGU

MAENEO mengi ya Kaunti ya Lamu ni visiwa ambavyo vimezingirwa na Bahari Hindi. Hivyo, usafiri huwa kwa vyombo vya majini ikiwemo boti, mashua, jahazi, mitumbwi miongoni mwa vingine vya asili.

Visiwa kama Lamu, Shella, Pate, Faza, Mtangawanda, Kizingitini, Ndau, Mkokoni, Kiwayu hushuhudia kiwango kikubwa cha usafiri.

Kwa jumla kuna zaidi ya visiwa 35 katika Kaunti ya Lamu.Wakati mwingi wageni katika kisiwa hicho ambao wana jicho pevu hawatakosa kubaini kuwa, boti na mashua wanazotumia zimepewa majina ya mvuto wa kipekee.

Kwa mfano, utapata boti kwa jina ‘Shani ya Lamu’, ‘Lamu Tamu’, ‘Haufungwi’, ‘Samaki Mkuu’, ‘Tusitiri’ na kadhalika.

Hii ni desturi ambayo imekuwepo tangu jadi, ila wageni wengi katika kaunti hiyo huwa hawafahamu ni mbinu gani hutumiwa na wamiliki wa vyombo hivyo kuvitaja majina, wala kama yana maana yoyote fiche.

Taifa Leo imebainisha kuwa, utoaji wa majina kwa boti za Lamu ni sanaa ambayo inahitaji kufanywa kwa makini.

Hii ni kutokana na kuwa wamiliki na wahudumu wa vyombo hivyo wanaamini kwamba ni kupitia majina hayo ambapo boti au mashua yao itawaletea baraka wanapokuwa katika shughuli zao baharini.

Katika mahojiano, baadhi yao walieleza kuwa kigezo cha kwanza ambacho watengenezaji na wamiliki wa maboti na mashua huzingatia katika kupeana majina kwa vyombo vyao vya usafiri wa baharini ni maandhari na sifa za Lamu, imani za kidini au hata mahaba kwa wapenzi wao.

Kwa mfano, kuna mashua ambayo jina lake ni ‘Lamu Tamu’. Hii ina maana ya moja kwa moja kwamba Lamu ni eneo lililo na ladha nzuri ya kuvutia.

Kulingana na Bw Ali Omar ambaye ni msanii wa kutoa majina kwa vyombo vya baharini Lamu, mashua kwa jina ‘Lamu Tamu’ imekuwa ikipendwa na wageni wengi, watalii na hata wenyeji.Kulingana naye, jina hilo hufanya abiria wa chombo hicho waamini litawawezesha kupata utamu halisi wa kisiwa cha Lamu.

“Mashua ya Lamu Tamu niliipa jina hilo kutokana na msemo wa tangu jadi eneo hili wa ‘Lamu Tamu, Atakao Nae’; kumaanisha Lamu ni yenye ladha tamu ya kupendeza na yeyote anayetaka kuja Lamu aruhusiwa.

“Kwa sababu hiyo, mashua yenyewe imeibukia kupendwa na kila mmoja, hasa wageni na watalii wanaozuru hapa. Matokeo yake ni biashara ya usafiri kunoga kila uchao,” akasema Bw Omar.

Boti nyingine ambayo Taifa Leo ilibaini asili ya jina lake la kipekee ni ‘Haufungwi’.Kulingana na msanii mwingine wa majina ya vyombo vya baharini mjini Lamu, Bw Mohamed Mote, jina ‘Haufungwi’ lina maana kwamba mlango wa rehema haufungwi.

Bw Mote anasema manahodha wengi wamekuwa wakitumia mashua hiyo kufanyia kazi zao za siku, kwani wanalinganisha jina lake na imani kuwa Mungu Mwenyewe ndiye hupeana riziki na kwamba hata binadamu akajaribu kwenda kinyume namna gani kuiziba bahati yako, ikiwa bahati hiyo ya Mungu imepangwa kukufikia itakuteremkia tu.

“Haufungwi ni jina linaloleta matumaini makubwa kwa manahodha na hata wasafiri wanaotumia boti hiyo. Inamaanisha Baraka za Mungu hakuna anayeweza kuzizuia. Kama umepangiwa utapata Baraka zake Maulana basi utazipokea tu hata waja wakajaribu kuzizuia au kuziba mlango wako,” akasema Bw Mote.

Ukiwasili katika kisiwa cha Lamu pia utakaribishwa na mashua kubwa kwa jina ‘Tusitiri’.Taifa Leo ilibaini kuwa jina hili halikupeanwa kwa mashua hiyo tu kama pambo bali pia ni ombi rasmi kwa wanaotumia boti hiyo.

Ikumbukwe kwamba wasafiri wanaotumia Bahari Hindi hupitia dhiki nyingi katika safari zao, ikiwemo mawimbi makali, dhoruba na hata ajali.

Kulingana na msanii wa majina Ahmed Issa, jina ‘Tusitiri’ ni ombi ambalo mabaharia wengi huwa nalo mioyoni mwao wanaposafiri, wakimuomba Mwenyezi Mungu kuwalinda na kuwafikisha salama kule wanakoelekea.

“Wanapofika sehemu wanakoenda basi huwa wamesitiriwa kutokana na mikosi ya ajali na zahama za baharini, hivyo jina-Tusitiri,” akasema Bw Issa.

Subira pia ni neno lingine la Kiswahili ambalo limeonekana kwenye mashua Lamu. Subira maana yake ni uvumilivu.

Bw Abdalla Suleiman ambaye pia ni msanii wa majina ya vyombo vya baharini kwenye kisiwa cha Pate anasema msingi wa jina hilo ni jinsi baharia yeyote lazima awe na sifa ya ‘subira’, kumaanisha atavumilia hali ngumu akiwa safarini ili atimize kusudi la kufika kule anakokwenda.

Kwa hivyo mtu mwenye subira hata akabiliwe na changamoto za namna gani baharini atavumilia wala hawezi kufikia kiwango cha kukata tamaa.

Pia utapata boti iliyopewa jina ‘Nuru’ ambayo yamaanisha ‘mwangaza’ au miale.Bw Athman Abdi anasema yeye binafsi hupenda sana kuabiri mashua kwa jina ‘Nuru’ akiamini kwamba safari yake haitaghubikwa na giza hadi kufika pale anapoelekea.

Watengenezaji na wamiliki wa maboti pia hupeana majina kulingana na uwezo au ujasiri wa chombo husika.

Aghalabu utapata mashua kwa jina ‘Samaki Mkuu’. Samaki wakuu baharini ni kama vile nyangumi, papa na wengineo.

Sifa za samaki hao ni kwamba wako na ujasiri, nguvu na uwezo wa kutekeleza jambo.Ikumbukwe kwamba samaki kama vile papa na nyangumi pia huwa na sifa ya kuwa na kasi na uwezo wa kupasua mawimbi na dhoruba kali wanapozunguka bahari.

Bw Hassan Alwy ambaye ni msanii wa majina ya maboti na mashua eneo la Wiyoni, Kaunti ya Lamu anasema jina la mashua ‘Samaki Mkuu’ linadhihirisha jinsi boti hiyo ilivyo na nguvu, uwezo na kasi ya kupasua mawimbi kwenye bahari kuu inaposafirisha mabaharia.

Anasema wasafiri hupenda kutumia mashua hiyo kusafiri wakijua kuwa hakuna changamoto zozote zitakazopatikana baharini ambazo zitazuia mashua hiyo kuendelea na safari baharini.

“Ukiona tu jina Samaki Mkuu wazo litakalokupiga akilini kwa mara ya kwanza ni uwezo alio nao samaki mkuu. Mara nyingi samaki wakubwa hupatikana kwenye bahari ya kina kirefu iliyojaa mawimbi. Hii ina maana kwamba mashua husika iko na nguvu za kukabiliana na mawimbi hayo makubwa baharini na kuendelea na safari bila wasiwasi wowote,” akasema Bw Alwy.

Kuna boti au mashua ambazo pia hubandikwa majina kulingana na upendo ambao mwenye chombo hicho cha kusafiri yuko nao.

Wengine pia huzipa mashua na boti majina ya wanawake au wapenzi wao waliowasitiri moyoni kama mbinu mojawapo ya kuwaenzi au kuwakumbuka, iwe wako hai au wakiwa wamefariki.

Utapata majina ya kuvutia kama vile ‘Tausi,’ ‘Chaurembo,’ ‘Lazizi,’ ‘Sauda,’ ‘Kimwana,’ na kadhalika.

Kulingana na wasanii wanaobandika vyombo hivyo majina, watu hutaka kuvitaja wapenzi wao ili hata wanapokuwa mbali baharini wahisi wako pamoja nao.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Waliopigania ukombozi wasipuuzwe

Hamwezi kuzima hasla, Ruto aambia wapinzani