HabariSiasa

Dhahabu bandia yamfaa Ruto

May 20th, 2019 2 min read

PETER MBURU na ZACHEUS MWASAME

SAKATA ya dhahabu bandia imeanza kumfaa kisiasa Naibu wa Rais William Ruto, ambaye sasa anawakashifu vigogo wa NASA kwa masaibu ya kulaghaiwa ufalme wa Dubai.

Dkt Ruto aliyekuwa kwenye hafla ya kuchangia kanisa katika kaunti ya Bungoma, alidai kuwa alifahamu tangu zamani kwamba viongozi hao hawakuwa na msimamo wala maarifa ya kuiendeleza nchi.

Akizungumza bila ya kuwataja kinara wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetangula ambao wamehusishwa na sakata hiyo, Dkt Ruto alisema kama vile safari ya Kanani ilivyokuwa bandia, hata biashara wanayojihusisha wanasiasa hao ni bandia.

Sakata hiyo imevuta majina ya Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Hii ni baada ya kanda ya mawasiliano ya simu kufichuka, ambapo mtu anayeaminika kuwa Bw Wetang’ula wakizungumza na mwanamume mwingine wanajadili kuhusu sababu ya ‘dhahabu’ hizo zilikosa kufika, majina ya viongozi hao yakipenyeza katika mawasiliano baina yao.

“Walitwambia kuwa wanaenda Kanani lakini ikawa ya bandia, saa hii eti wanauza dhahabu, hiyo dhahabu tena ati ni ya bandia. Sasa hawa watu tunawajua, hakuna haja ya kusumbuana nao,” Dkt Ruto akasema.

Dkt Ruto alilaumu upinzani kuwa umekuwa ukijifanya kuwa safi, ilhali kichinichini unaendesha mambo ya ukora.

“Upinzani ulilaumu Jubilee kuwa iliiba Eurobond na kuwa tumeuza Bandari ya Mombasa, ambao ulikuwa uongo. Sasa wanauza dhahabu feki. Wakenya sasa wanajua wakora ni kina nani,” akasema.

“Viongozi wengine waache kujifanya kuwa watakatifu ilhali hao ni sehemu ya wale wanaohusika na biashara za vitu feki kama hiki kisa cha dhahabu,” akasema.

Jana, viongozi wa kisiasa walitumia suala hilo kuchafuana, kila upande ukipanga mwingine tope, nazo idara za uchunguzi wa uhalifu zikitakiwa kulichangamkia na kukamata washukiwa.

Wabunge waliokuwa wameandamana na Dkt Ruto walitumia fursa hiyo kutaka waliotajwa kuchunguzwa, bila kujali hadhi.

“Biashara zinatatizwa na watu ambao wanajihusisha na mambo ya ufisadi kwenye kisa cha dhahabu feki. Tunataka hatua kuchukuliwa kwa washukiwa bila kujali hadhi yao katika jamii,” akasema mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya.

Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga jana asubuhi naye alidai kuwa baadhi ya viongozi kutoka bonde la ufa ndio waliunda mpango wa kuhusisha majina ya Rais, waziri Matiang’i na Bw Odinga katika sakata hiyo, kwa sababu za kisiasa.

“Hao wabunge walitumwa kwa Zaheer (Jhanda, (mhusika mkuu katika sakata hiyo)) kuhusisha majina ya Rais, Raila na waziri Matiangi katika sakata hiyo lakini sasa mpango umejulikana. Ni wabunge watatu na gavana mmoja kutoka bonde la ufa,” akasema Bi Wanga.

Makabiliano ya kimaneno baina ya kambi za Dkt Ruto na Bw Odinga yalitawala jana, pande zote zikilauminana, makabiliano kwenye mitandao ya kijamii yakihusisha Bi Wanga, mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.

Katika kanda hiyo ya mawasiliano ya simu, sauti inayoaminika kuwa ya Bw Wetang’ula inamwambia mwenzake (anayeaminika kuwa Zaheer) kuwa alikuwa amewahusisha Rais, Bw Odinga na Waziri Matiang’i katika mpango huo wa kusafirisha dhahabu, akimhakikishia kuwa “hakutakuwa na jambo litakaloenda kombo ndugu yangu.”

Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji Jumamosi ilisema kuwa imeanzisha uchunguzi kuhusu sakata hiyo, lakini ikapuuza kuhusishwa kwa Rais, Bw Odinga na Dkt Matiang’i.