Habari Mseto

Dhamana ya Sh50,000 kwa kujifanya Jaji Ibrahim

March 18th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyejifanya kuwa Jaji Mohammed Ibrahim wa Mahakama ya Juu alishtakiwa Jumatatu katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Bw Henry Antony Wasike alikanusha shtaka la kuandikisha laini ya simu katika kampuni ya Safaricom akijifanya kuwa Jaji Ibrahim.

Shtaka dhidi ya Bw Wasike lilisema  mnamo Februari 26 mwaka huu mwendo wa saa tatu na dakika 14 asubuhi aliandikisha laini ya simu kwa kampuni ya safaricom akitumia jina la Jaji Mohammed Ibrahim wa Mahakama ya Juu.

Bw Wasike ambaye hakuwa amewakilishwa na wakili aliomba hakimu mkuu Bw Francis Andayi amwachilie kwa dhamana.

“Naomba mahakama iniachilie kwa dhamana,” mshtakiwa alimsihi Bw Andayi. Kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi hakupinga kuachiliwa kwa mshtakiwa kwa dhamana.

“Dhamana ni haki ya kila mshukiwa kwa mujibu wa kifungu nambari 49 cha katiba,” alisema Bi Kirimi. Bw Andayi aliamuru mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu.

Kesi dhidi ya mshtakiwa ilitengwa kusikizwa Mei 6 mwaka huu. Watatu wameorodheshwa kufika mahakamani kutoa ushahidi.

Mahakama  iliamuru kiongozi wa mashtaka ampe mshtakiwa nakala za ushahidi ndipo aandae ushahidi wake.

Kesi itatajwa Mei 29 upande wa mashtaka uthibitishe ikiwa umempa mshtakiwa nakala za mashahidi kisha maagizo zaidi yatolewe.