MakalaSiasa

Dhamira kuu ya Miguna Miguna yaonekana ni kujitakasa apate umaarufu kisiasa

February 11th, 2018 3 min read

Wakili maarufu na mwanasiasa wa NASA aliyefurushwa humu nchini hadi nchini Canada Dkt Miguna Miguna. Picha/ Maktaba

Na WANDERI KAMAU

Kwa Muhtsari:

  • Wachanganuzi wasema kwamba urejeo wa Dkt Miguna katika kambi ya Bw Odinga huenda ukawa hatua ya kujijenga upya kisiasa
  • Viongozi wengi ambao wanalenga kumrithi Bw Odinga walinyamaza wakati Dkt Miguna akiziuiliwa na polisi
  • Dkt Miguna hajapokelewa vizuri katika eneo la Nyando anakotoka, kwa madai ya kuwa “msaliti mkubwa”
  • Baadhi ya watu wanamwona kama mnafiki, anayelenga kujijenga kisiasa kwa kutumia jina la Bw Raila Odinga

HATUA ya wakili mbishi na kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM), Dkt Miguna Miguna kujitokeza kama ‘mtetezi mkuu’ wa kinara wa NASA Raila Odinga, ni mkakati wa kurejesha umaarufu wake miongoni mwa jamii ya Waluo.

Wachanganuzi wanasema kwamba urejeo wa Dkt Miguna katika kambi ya Bw Odinga huenda ukawa hatua ya kujijenga upya kisiasa, hasa baada ya kushindwa kwenye kinyang’anyiro cha ugavana katika Kaunti ya Nairobi mnamo Agosti 8, 2017.

Dkt Miguna Miguna amewahi kuwa mkosoaji mkuu wa Bw Odinga, ila ni baada ya Agosti 8, ambapo alirejea katika kambi yake, akiapa kupigania ‘haki’ baada NASA kudai kwamba ‘ilinyang’anywa’ ushindi wake na mrengo wa Jubilee.

“Maamuzi ya Miguna Miguna kumtetea Odinga ni mkakati wa kuimarisha umaarufu wake kitaifa, na kurejesha urafiki na jamii yake ya Waluo. Hii ni kwa kuwa kwa mtazamo wa wengi alikuwa ‘amepoteza’ mwelekeo kisiasa, hasa baada ya kukosana na Bw Odinga mnamo 2011,” asema Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Kulingana na Bw Muga, hatua ya Bw Miguna kujitokeza kama kiongozi wa pekee mwenye “ushujaa” katika kumlisha kiapo Bw Odinga mnamo Januari 30, ni mkakati mpana wa mchakato wa urithi wa kisiasa wa Bw Odinga.

Bw Miguna alirejeshwa kwa lazima nchini Canada na Serikali  Jumatano usiku, kwa sababu ya kushiriki katika kiapo hicho, ambacho kimefasiriwa kama “tishio kwa usalama wa kitaifa.”

Aidha, mchanganuzi huyo anarejelea “ukimya” uliodhihirika miongoni mwa viongozi wakuu wa NASA, akiwemo Bw Odinga mwenyewe, Seneta James Orengo wa Siaya, wabunge Junet Mohammed (Suna Mashariki), John Mbadi kati ya wengine kama ishara ya wazi kuhusu ‘tishio za kisiasa’ wanazokabiliwa kutoka kwa kupanda kwa nyota ya Bw Miguna.

 

NASA haikumtetea

Kama kile kinaonekana kudhihirisha hayo, wakili Edward Sifuna, ambaye alimwakilisha Bw Miguna, alikubali kwamba viongozi wengi ambao wanalenga kumrithi Bw Odinga walinyamaza wakati akiziuiliwa na polisi.

“Hatukuchukua juhudi za kutosha kama Bw Miguna. Alibaki kujitetea peke yake huku baadhi yetu tukitazama tu,” akasema Bw Sifuna, aliyeonekana kutoridhishwa na mikakati ya NASA kumtetea Bw Miguna.

Kwa hayo, wachanganuzi wanafasiri ukimya huo kama hofu iliyo na baadhi ya viongozi hao kuhusu umaarufu mkubwa ambao Bw Miguna amepata kutokana na ujasiri wake kumwapisha Bw Odinga.

Mchanganuzi wa kisiasa Edward Kisiang’ani  asema kwamba NASA haikuonyesha umoja kamili na kujitolea kwake, wakati mmoja wao alijipata taabani.

“Ni dhahiri kwamba viongozi wa NASA hudumisha umoja mkubwa, kila wakati mmoja wao anapokamatwa, au anakabiliwa kisiasa kwa njia yoyote. Tulitarajia kuwaona akina Orengo, Muthama kati ya wengine wakijitokeza vikali kuilaumu serikali dhidi ya ‘maonevu dhidi ya mmoja wao. Lakini hali ilikuwa tofauti. Walinyamaza!” asema mchanganuzi huyo.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, Bw Miguna alishindwa kunyakua ugavana katika Kaunti ya Nairobi, alipowania kama mgombea huru.

 

‘Msaliti mkubwa’

Bw Miguna pia hajakuwa akipokelewa vizuri katika eneo la Nyando (anakotoka), Kisumu katika eneo la Nyanza, kwa madai ya kuwa “msaliti mkubwa” wa Bw Odinga, hasa baada ya kuandika vitabu Peeling Back the Mask: A Quest for Justice in Kenya na Kidneys for The King: De-forrming the Status  Quo’ ambavyo vilimkosoa sana Bw Odinga.

Kwa wakati mmoja, aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Bw Fred Outa, aliwaongoza wakazi kuandamana dhidi ya Bw Miguna, ambapo pia walichoma mfano wa “jeneza” lake kwa kuwa msaliti.

Kwa upande wake, Bw Miguna alikosoa vikali kisa hicho, akikifananisha na “amri iliyotolewa” na Bw Odinga.

Hata hivyo, hali imeonekana kuwa tofauti mara hii, ambapo wakazi waliandamana vikali wakiilaumu serikali dhidi ya kumhangaisha Bwe Miguna, waliyemtaja kuwa “mtoto wao.”

Hivyo, wachanganuzi wanasema kwamba ingawa huenda Bw Miguna hatimaye akafaulu kupata uungwaji mkono katika jamii hiyo, juhudi zake hazitakosa pingamizi, hasa kutoka kwa viongozi ambao watahisi kutishwa na urejeo wake.

 

Hajakubalika kama ‘Jenerali’

Mdadisi wa kisiasa Kiprotich Mutai asema kwamba makovu ya usaliti wa Bw Odinga na Bw Miguna, hasa baada ya matamshi yake ya awali dhidi ya Bw Odinga. “Kuna viongozi ambao bado hawajamkubali Bw Miguna kama ‘Jenerali’  wao wa kisiasa.

Baadhi wanamwona kama mnafiki, anayelenga kujijenga kisiasa kwa kutumia jina la Raila, kama wengi ambavyo wamekuwa wakifanya ili kupata upenyu katika siasa za kitaifa,” asema Bw Mutai.

Licha ya hayo, Bw Miguna amekuwa akijinadi kama “mwanamapinduzi” anayelenga kuhakikisha kwamba haki kamili imepatikana kwa wale ambao wamekuwa wakibaguliwa kisiasa.

“Lengo langu ni kulainisha mfumo wa kisiasa nchini. Tulipigana na utawala wa rais mstaafu (Moi) na kumshinda. Kamwe hatutakubali kutishwa na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Willam Ruto,” akasema Bw Miguna.