Makala

UKUMBI WA LUGHA: Dhana ya Isimu na Isimu Jamii

February 18th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KATIKA makala ya leo tutachunguza na kuchambua kwa kina dhana ya Isimu na Isimu Jamii katika Kiswahili.

Ni vyema kufahamu kwamba japo  isimu na isimu jamii ni taaluma mbili zinazotofautiana kimsingi taaluma hizi hukamilishana pakubwa.

 

Chimbuko la Isimu Jamii

Kwa mujibu wa Mekacha (2000), taaluma ya isimu jamii ilianza Marekani katika miaka ya 50 na 60.

Waasisi wa taaluma hii ni pamoja na wanasosiolojia kama vile Fishman (1971), wanaanthropolojia kama vile Del Hymes (1972) na wanaisimu mathalan akina Labov William (1972), Gumperz (1972) na Bright William (1965).

Azma ya wataalam hawa ilkuwa kubaini tofauti za tamaduni ngeni huko Marekani ambapo kulikuwepo na Wamarekani wenye asili ya Kiafrika na Wamarekani Wahindi (Wahindi Wekundu). Wataalam hawa walitaka kuzifahamu tamaduni hizo ngeni ili waweze kuzitumia katika elimu.

Msanjila na wenzake (2011) katika kufasili dhana ya isimu jamii wanasema kwamba wataalamu mbalimbali wa lugha wanakubaliana kimsingi kwamba isimujamii ni taaluma inayoshughulika na uchunguzi unaolenga kufafanua uhusiano uliopo kati ya isimu na jamii mathalan Trudgill 1983; Hudson 1985 na Mekacha 2000.

Isitoshe, Msanjila na wenzake wanaendelea kusema kuwa, ‘kwa kifupi isimujamii ni taaluma inayoshughulikia matumizi ya lugha katika jamii. Kwa muhtasari, taaluma hii inajaribu kuelezea uhusiano uliopo baina ya lugha na jamii.’ Kwa mtazamo huu ni wazi kwamba kuna uhusiano mkubwa sana baina ya lugha na jamii.

Wataalamu wengine wanaoonekana kupigia upatu mtazamo huu ni kama vile Besha (2007:13) anayesema kuwa, isimujamii ni utanzu unaojishughulisha na uchunguzi jinsi lugha inavyotumika katika jamii.

Aidha, King’ei (2010:1) anasema Isimu Jamii ni taaluma inayoeleza uhusiano wa karibu uliopo kati ya matumizi ya lugha na maisha ya jamii. Vilevile wataalam wengi wanaonekana kuwa na muelekeo sawa katika kufasili dhana ya isimu, kwani wengi wao wanakubaliana kwamba, Isimu ni taaluma ya ufafanuzi, uchambuzi na uchunguzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi mathalan Massamba 2004:19; Mgullu 1990:1 wakiwarejea wanaisimu mbalimbali kama vile Richard na wenzake 1985.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo:

   Msanjila, Y. P. (1990) “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

   Mtembezi, I. J. (1997) “Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia”. Dar es Salaam: BAKITA.

   Mulokozi, M. M. (1991) “English versus Kiswahili ni Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studies Ghent.