Dhuluma: Mbunge ahimiza wanawake wazungumze waziwazi badala ya kujitia unyongeni

Dhuluma: Mbunge ahimiza wanawake wazungumze waziwazi badala ya kujitia unyongeni

Na KALUME KAZUNGU

MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo, amewahimiza wanawake wanaopitia dhuluma za aina yoyote kuripoti visa hivyo kwa polisi na pia kwa ofisi yake ili hatua mwafaka za kisheria zichukuliwe dhidi ya wanaowadhulumu.

Kulingana naye, tamaduni zilizopitwa na wakati, dini na umaskini ni miongoni mwa sababu kuu zinazozuia wakazi wa Lamu kuripoti visa vingi vya dhuluma za kijinsia miongoni mwa wanawake na wasichana.

Akizungumza mjini Lamu wakati wa hafla ya kukabidhiwa kwa hundi ya Sh6 milioni kutoka kwa Halmashauri ya Bandari nchini (KPA) za kujengea kituo cha wanaodhulumiwa kijinsia, Bi Obbo alisema wanawake wengi na wasichana wamelazimika kuvumilia mateso kutoka kwa wanaume ili kuepuka aibu na pia kuogopa kunyimwa huduma za kimsingi.

Bi Obbo aliitaka jamii ya Lamu kuepuka kujihusisha na dhuluma za wanawake na wasichana na badala yake kuwapa nafasi wanawake kujiendeleza.

Bi Obbo aidha alisifu hatua ya KPA ya kupeana fedha za ujenzi wa kituo cha kuwahifadhi wanawake na wasichana wanaodhulumiwa Lamu, akisisitiza kuwa kuwepo kwa kituo hicho kutasaidia kuangazia na hata kupunguza au kukomesha kabisa dhuluma za kijinsia miongoni mwa jamii kote Lamu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa KPA, Rashid Salim alisema walionelea kutoa fedha hizo za ujenzi wa hifadhi hiyo kama njia mojawapo ya kuisadia jamii ya Lamu na kuendeleza uhusiano mwema kati ya KPA na jamii.

Bw Salim alisema pia wametoa zaidi ya laki sita ili kusaidia kuendeleza soka kwa vijana wa Lamu na kuwaepusha kujiingiza kwenye uraibu wa dawa za kulevya.

You can share this post!

Wakazi 3,500 Mwatate hatarini kufurushwa

Madereva, wamiliki wa tuk-tuk waandamana Mombasa kwa...