Dhuluma za ngono zinavyotatiza utalii

Dhuluma za ngono zinavyotatiza utalii

Na WAANDISHI WETU

KESI ya mfanyabiashara Asif Amirali Alibhai Jetha, ambaye alihukumiwa miaka 30 gerezani, imezidi kufichua jinsi dhuluma dhidi za wasichana na wanawake Pwani hutumiwa kama kivutio cha watalii wanaotafuta burudani haramu.

Jetha alipatikana na hatia ya kuwaleta nchini wanawake 12 raia wa Nepal kiharamu akawafanya watumwa wa ngono na kuwatumia kibiashara kinyume na sheria za nchi na za kimataifa.

Kesi hiyo ilionyesha jinsi biashara aina hiyo zinavyoendelea bila kuingiliwa na maafisa wa usalama.

Kulingana na wanawake waliotoa ushahidi katika kesi yake, Jetha alikuwa akilenga wasichana kutoka kwa familia maskini Nepal.

Walieleza kuwa, wote walikuwa katika hali mbaya kimaisha nchini mwao na walihitaji ajira kwa hivyo walipoahidiwa kazi nchini Kenya ambapo waliambiwa wangetajirika kwa kusakata dansi vilabuni, hawakuwaza mara mbili.

Kulingana nao, waliahidiwa kazi katika kilabu cha burudani cha New Rangeela mjini Mombasa.

Wanawake hao waliambia mahakama kuwa walifanyishwa kazi kila siku na kupewa siku moja pekee kwa mwezi kupumzika.

Hawakukubaliwa kuwa na simu na waliruhusiwa tu kutumia simu na kijakazi wa nyumba yao kati ya saa tisa mchana na saa kumi na mbili jioni kuwasiliana na familia zao pekee.

Ilisemekana kuwa, kilabu hicho hutumiwa tu na matajiri kwani ada za kiingilio na bei za bidhaa na huduma, ikiwemo huduma zinazotolewa na wasichana hao, ni za juu mno.

Katika mahakama za Mombasa, kuna kesi nyingine kama hii ambazo bado zinaendelea kusikilizwa huku nyingine zikiwa zishatolewa hukumu.

Mojawapo ya kesi hizo inahusu raia wawili wa Israeli, Ashush David na Koren Avraham, ambao walipatikana wakiwa wameficha watoto wawili wa miaka 14 na 15 katika nyumba iliyo mtaa wa Bamburi.

Ripoti ya uchunguzi ilionyesha kuwa, walikutana na watoto hao katika ufuo wa bahari ya Copa Cabana kabla kuwahadaa kwa pesa na zawadi nyingine kama vile simu, kisha kuwapeleka Bamburi na kuwadhulumu kingono.

Katika mwaka wa 2019, raia wa Ujerumani na mwenzake wa Ukraine walishtakiwa kwa kumshambulia mwanamke, kumvua nguo na kunasa video zake akiwa uchi.

Ilisemekana kuwa, mwanamke huyo alikuwa amewasiliana nao kupitia mtandaoni kabla kwenda kukutana nao Mtwapa ambapo, baada ya kufurahia vyakula na vinywaji, walimkataza kuondoka ndipo wakamshambulia.

Kesi nyingine ilimhusu Panciano Renato, 75, ambaye alishtakiwa kwa kumnajisi mtoto wa shule ya msingi nyumbani kwake Mtwapa.

Ripoti ya polisi ilidai kuwa, mwanafunzi huyo wa darasa la saba alikuwa ameendea karo alizokuwa ameahidiwa lakini akaleweshwa kisha kunajisiwa.

Katika mwaka wa 2018, Keith Morris, 72, ambaye ni raia wa Uingereza, alihukumiwa miezi 18 gerezani na Mahakama ya Uingereza baada ya kupatikana na hatia ya kuwadhulumu kingono watoto wanane katika Kaunti ya Kilifi.

Mapema 2014, Perniaux Allain Robert, raia wa Ubelgiji alihukumiwa miaka 20 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi msichana wa miaka 12.

Katika kesi nyingi, wasichana huwa wametoka katika familia maskini na huhadaiwa kwa pesa au aina nyingine za misaada.

Baadhi ya wazazi pia hushtakiwa kwa kutelekea majukumu ya kulea watoto wao, ikidaiwa baadhi yao hata huruhusu wazee kuwachukua watoto wao ili wapate pesa za kujikimu.

You can share this post!

Mtihani kwa Uhuru kipindi cha lala salama

CHARLES WASONGA: Kaunti zisipodhibitiwa nchi itaisha kwa...

T L