Dhuluma zinadumaza wanawake kisiasa – Ripoti

Dhuluma zinadumaza wanawake kisiasa – Ripoti

NA MARY WANGARI

VISA vya dhuluma na ubaguzi wa kijinsia vinavyowakabili wagombea wanawake nchini vinanuiwa kuwavunja moyo na kuwafanya kujiondoa katika ulingo wa siasa, ripoti mpya imesema.

Kuanzishwa kwa nyadhifa za wanawake kwenye ulingo wa kisiasa kulikofanikishwa na Katiba Mpya ya 2010 kumechangia kuongezeka pakubwa kwa visa vya dhuluma dhidi ya wagombea wanawake, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu (FIDH) kwa ushirikiano na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KHRC).

Kulingana na ripoti hiyo, utekelezaji wa sheria kuhusu nyadhifa za wanawake hasa katika mazingira ya kisiasa ambapo ubaguzi wa kijinsia umekolea, umechochea aina mbalimbali za dhuluma na pingamizi dhidi ya ujumuishaji wa wanawake katika siasa kwa lengo la kuwatamausha.

“Maendeleo haya ya kisiasa yamesababisha uhasama wa kijinsia katika juhudi za kuwazuia wanawake kuchaguliwa katika nyadhifa za uongozi zilizokuwa awali zikitawaliwa na wanaume.

Kuanzia kwa vitedo vya ukatili, dhuluma hadi ubaguzi wa kijinsia katika tasnia za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, huelekezewa wanawake kwa lengo la kuwafanya wajiondoe katika maisha ya siasa,”

“Katika mazingira ya Kenya, watafiti walibaini kuwa dhuluma zinazoelekezewa wanawake katika siasa, ni sehemu mojawapo ya juhudi za kina za kuwanyima wanawake fursa ya kupenya katika nyadhifa za kisiasa ambazo kulingana na tamaduni zimekuwa zikitawaliwa na wanaume,” yasema ripoti hiyo.

Japo usawa wa kijinsia bado haujafanikishwa, idadi kubwa ya wanawake wanazidi kupenyeza kwenye nyanja za siasa na kuchaguliwa au kuteuliwa kama wawakilishi wanawake, wabunge, maseneta na hata magavana.

“Visa vya wanasiasa wanawake nchini wanaokabiliwa na aina mbalimbali za dhuluma za kijinsia vimerekodiwa. Tangu kuidhinishwa kwa Katiba Mpya 2010 na kuanzishwa kwa nyadhifa za kuchaguliwa au kuteuliwa, dhuluma dhidi ya wanasiasa wanawake zimeongezeka pakubwa hususan msimu wa uchaguzi, kukiwa na ripoti za wanawake kushambuliwa kwa matusi na kupigwa hata na wanasiasa wenzao wa kiume,” inaongeza ripoti hiyo.

Mashirika hayo yameelezea hofu kuwa, iwapo serikali haitachukua hatua ya dharura, huenda visa vya dhuluma za kijinsia ambavyo vimeshuhudiwa kupitia machafuko ya baada ya chaguzi zilizopita vikashuhudiwa kwa mara nyingine mwaka huu.

Utafiti uliofanywa na mashirika hayo vilevile uliashiria kuwa idadi kubwa ya visa vya dhuluma za kijinsia vilifanyika katika ngome za upinzani hususan kaunti za Kisumu, Migori na Vihiga.

Jumla ya wanawake 79 wenye umri wa miaka 45 kwenda chini waliohojiwa, walithibitisha kuwa idadi kubwa ya waliotekeleza dhuluma hizo za kijinsia ni maafisa wa polisi.

“Idadi kubwa ya wanawake waliohojiwa na FIDH na KHRC waliripoti kuwa hawana hamu tena ya kushiriki mchakato wa uchaguzi. Baadhi ya wahasiriwa waliashiria kuwa hawatapiga kura tena kwa kuhofia maisha yao na familia zao,” ikasema.

“Hali kwamba maafisa wa serikali ni miongoni mwa waliohusika na kuhatarisha usalama kwa vitendo vya dhuluma za kijinsia bila kuchukuliwa hatua, inachangia zaidi kuwazuia wanawake kujihusisha na maisha ya siasa.

Katika hali fulani, hii inahujumu hatua zilizofanikishwa kwa miaka iliyopita zinazolenga kufungua nafasi za wanawake kushiriki katika mchakato wa siasa,” ikanukuliwa.

  • Tags

You can share this post!

Watu wachache wajitokeza kujiandikisha IEBC ikisaka kura...

Maalim aahidi kupambana na utovu wa usalama Bonde la Ufa

T L