Michezo

Di Maria kukosa mechi nne kwa utovu wa nidhamu

September 24th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ANGEL Di Maria wa Paris Saint-Germain (PSG) amepigwa marufuku ya mechi nne kwa kuchangia vurugu katika mechi iliyowakutanisha na Olympique Marseille kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Septemba 13, 2020.

Di Maria, 32, alipatikana na hatia ya kumtemea mate kimakusudi beki wa Marseille, Alvari Gonzalez wakati wa mechi hiyo iliyoshuhudia jumla ya wanasoka watano wakionyeshwa kadi nyekundu.

Fowadi huyo raia wa Argentina ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Manchester United, alikuwa miongoni mwa wanasoka saba wa PSG waliokuwa wameugua Covid-19 kabla ya kusakatwa kwa gozi.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Ufaransa, Di Maria alikuwa na hatia na alihatarisha maisha ya Gonzalez, maafisa wa mechi, makocha na mashabiki waliohudhuria mchuano huo.

Mbali na Di Maria, wachezaji Neymar, Leandro Paredes na Layvin Kurzawa wa PSG; pamoja na Jordan Amavi na Dario Benedetto wa Marseille ndio walioonyeshwa kadi nyekundu kwa kuhusika katika fujo hizo mwishoni mwa kipindi cha pili.

Akiondoka uwanjani, Neymar alimweleza msaidizi wa refa kwa fujo hizo zilichochewa na matukio ya ubaguzi wa rangi yaliyoendelezwa na wachezaji wa Marseille uwanjani.

Baadaye, fowadi huyo raia wa Brazil aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba “majuto ya pekee” aliyo nayo ni kwamba hakupata fursa ya kumtandika Gonzalez ambaye ni beki raia wa Uhispania kofi kali la usoni. Kesi inayohusisha matamshi hayo ya Neymar kwa Gonzalez itasikiliwa Septemba 30, 2020.

Marufuku dhidi ya Di Maria yanaanza kutekelezwa mnamo Septemba 29, 2020.