HabariKimataifa

Diamond akamatwa kwa kujionyesha akifanya 'mambo' kitandani na Hamisa

April 17th, 2018 2 min read

Na MWANANCHI

MSANII nyota wa Bongo Naseeb Abdul Juma, almaarufu Diamond Platnumz alikamatwa na kuhojiwa na polisi Jumatatu, kwa madai ya kusambaza picha za aibu mtandaoni zinazokiuka maadili.

Waziri wa Habari, Harrison Mwakyembe, Jumanne alisema msanii Diamond Platnumz alikamatwa baada ya video iliyomwonyesha akiwa na mwanamitindo Hamisa Mobeto kitandani kuchipuza katika mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo, msaanii huyo wa Bongo alionekana akipigana pambaja na Bi Mabeto ambaye ni mama ya binti yake.

Katika video hiyo, Diamond anasikika akimtania Mabeto kwa kumpeleka mahakamani kwa kutelekeza mtoto ilihali walikuwa kitandani pamoja wakati huo.

Lakini Mabeto Bi anamjibu kwa kusema, “Niache kwani bado nimekukasirikia.”

Video hiyo iliwavutia wengi huku baadhi wakikosoa Diamond kwa kujionyesha mitandaoni akifanya mapenzi kitandani na mpenziwe Mobeto.

Akizungumza bungeni Jumanne, Waziri Mwakyembe alisema serikali imebuni sheria inayozuia wasanii na Watanzania dhidi ya kutundika picha za uchi na kuchapisha mambo yanayokiuka utamaduni na maadili ya Kitanzania.

Waziri Mwakyembe pia aliagiza polisi kumkamata msanii wa kike anayejulikana kama Nandy baada ya picha zake zinazokiuka maadili kuchipuza mtandaoni.

Katika picha hizo, msanii Nandy anaonekana akimpiga busu mpenzi wake wa zamani anayefahamika kwa jina la Billnass.

Picha hizo zinadaiwa kupigwa 2016 lakini zilichipuza mtandaoni mwezi huu. Bw Mwakyembe alisema: “Tanzania sio jalala la kutupa picha za uchi zinazokiuka maadili yetu ya Kitanzania.”

Waziri alifichua kukamatwa kwa Diamond alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Ulanga Godluck Mlinga aliyetaka kujua serikali ilikuwa na mkakati gani kukomesha tabia za baadhi ya watu wanaotumia mitandao vibaya na kueneza ushoga.

Alisema ongezeko la Watanzania wanaotia picha za uchi mitandaoni linatokana na athari ya utamaduni wa mataifa ya ughaibuni hivyo akaahidi kukabiliana vikali na tatizo kwa kutumia sheria mpya.

Waziri Mwakyembe alilalama kuwa wasanii wa Bongo hawajakuwa wakipeleka nyimbo zao kuhaririwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kabla ya kuanza kuzicheza hadharani.

Msanii Diamond alitoa video hiyo tatanishi saa chache baada ya kuachilia wimbo mpya ‘Kwangwaru’ ambao amemshirikisha msaani mwenzake wa Bongo Harmonize.

Katika wimbo huo Diamond amemkejeli mpenziwe wa zamani, Zari ambaye amemwambia ‘Ukiachwa Achika’.

Diamond na Zari wamezaa pamoja watoto wawili; Tiffah na Nillan.