Michezo

DIAMOND LEAGUE: Mbivu na mbichi kubainika wanariadha wa Kenya wakilenga kutikisha dunia

August 13th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANARIADHA wanne mabingwa wa dunia kutoka Kenya wakiongozwa na mfalme wa mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot, wanatarajiwa kuibua msisimko mkubwa katika kivumbi cha Wanda Diamond League kitakachoanza Ijumaa usiku kwa duru ya Herculis kitakachotifuliwa katika uwanja wa Stade Louis II jijini Monaco, Ufaransa.

Hellen Obiri (mita 5,000), Beatrice Chepkoech (mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji) na Ferguson Rotich (mita 800) watatoana jasho na wapinzani wengine katika fani zao katika mbio za kwanza za kimataifa tangu janga la corona livuruge kalenda ya mashindano mbalimbali ya msimu huu.

Cheruiyot anayejivunia muda wa dakika 3:28.41 katika mbio za mita 1,500 atapania kulipiza kisasi dhidi ya Jakob Ingebrigtsen ambaye kwa pamoja na kaka zake Filip na Henrik, walimlemea katika mbio za mita 2,000 za Maurie Plant Memorial zilizoandaliwa sambamba katika uwanja wa Nyayo Nairobi na jijini Oslo, Norway mnamo Juni 11, 2020.

Cheruiyot ambaye ametawala mbio za mita 1,500 kwenye Diamond League kwa misimu mitatu iliyopita, alitamalaki Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar mnamo 2019 kwa muda wa dakika 3:29.26 mbele ya Taoufik Makhloufi wa Algeria (3:31.38) na Marcin Lewandowski kutoka Poland (3:31.46).

Yomif Kejelcha wa Ethiopia na Wakenya Vincent Keter na Timothy Sein watakuwa kati ya wapinzani wengine 13 wa Cheruiyot.

Obiri ambaye pia ni bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola, atalenga kumpiku Chepkoech katika mbio za mita 5,000 ambazo pia zimemvutia Mholanzi Sifan Hassan aliyetamalaki mbio za 1,500 na mita 10,000 katika Riadha za Dunia za Doha, Qatar mwaka jana.

Chepkoech ndiye mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi. Muda wake bora katika mbio hizi za mizunguko 12 na nusu ni dakika 14:39.33 aliouandikisha jijini Brussels, Ubelgiji mnamo 2017.

Mkenya Winny Chebet ambaye ni bingwa wa Afrika katika mita 1,500, Letesenbet Gidey wa Ethiopia na Mjerumani Konstanze Klosterhalfen ambaye ni mshindi wa shaba katika mita 5,000 duniani, wataazimia pia kuunga njama ya kubwaga Obiri atakayekuwa akitetea ubingwa wa Monaco baada ya kutawala kitengo hiki kwa mara ya mwisho mnamo 2017.

Mbio hizi zitanogeshwa pia na Mwingereza Laura Muir na mabingwa wa dunia katika mbio za mita 800, Halimah Nakaayi na Winnie Nyanyondo kutoka Uganda.

Rotich ambaye pia ni mshindi wa medali ya fedha na shaba duniani katika mbio za mita 800, alitawala kitengo hiki kwenye Diamond League mnamo 2017. Atapimana ubabe hii leo na Brazier Donavan Amerika na Amel Tuka kutoka Bosnia.

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Leonard Bett atakuwa mwakilishi wa pekee wa Kenya katika kitengo hiki baada ya gwiji wa mbio hizi Conseslus Kipruto kuugua Covid-19. Wapinzani wake wakuu watakuwa Soufiane El Bakkali wa Morocco na Waethiopia Getnet Wale na Lamecha Girma.

Chipukizi Jacob Krop na Nicholas Kimeli watatoana jasho na bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 Joshua Cheptegei kutoka Uganda. Cheptegei pia ni bingwa wa dunia, Jumuiya ya Madola na riadha za nyika katika mita 10,000. Mbio hizi za mita 5,000 zimemvutia pia Mkenya raia wa Uswisi, Julien Wanders anayejivunia muda bora wa dakika 13:1.84.

Malkia wa mbio za mita 1,500 kwenye Olimpiki 2016 Faith Chepngetich atagombea taji la mbio za mita 1,000 ambazo pia zitanogeshwa na Nanyondo, Nakaayi na Muir.