Makala

DICKSON MAJIMBO: Turuhusiwe kurekodi filamu popote tupendapo nchini

May 25th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ANAAMINI kwamba anaendelea vizuri anakolenga kuibuka miongoni mwa wana maigizo tajika hapa nchini miaka ijayo.

Anasema sekta ya filamu hapa nchini inaendelea kupiga hatua ambapo wasanii wa Kenya wanazidi kufukuzia wanaofanya kweli katika mataifa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.

Ingawa hajapata mashiko kulingana na matarajio yake anasema amejifunga nira kushiriki uigizaji kuhakikisha ametinga upeo wa juu.

Hakika wahenga hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa waliposema ”mwanadamu utamani kufika kiwango fulani maishani lakini hawezi bila wakati mwafaka kuwadia.’

Dickson Show Majimbo maarufu Mcee Show ama Senior Wrong Number alianza kujituma katika masuala ya maigizo mwaka 2013.

”Kwa sasa nimezamia zaidi masuala ya burudani maana mimi ni mwigizaji, mratibu wa sherehe (MC) pia mchekeshaji,” alisema na kuongeza kwamba anatamani kuwa mwimbaji wa nyimbo za injili miaka ijayo.

SISIMKA AFRIKA

Anadokeza kuwa alitambua talanta yake tangia akisoma shule ya Msingi kwa kuzingatia alikuwa alishiriki michezo ya kuigiza shuleni.

Mwigizaji huyu aliyekuwa akiandaa kipindi cha Sisimka Afrika kwenye runinga ya BrandPlus anasema anajivunia kushiriki filamu nyingi tu tangu aanze kujituma katika jukwaa la burudani.

Mcheshi huyu anajivunia kushiriki filamu kama ‘Bebabeba (NTV),’ ‘Junior (KTN),’ ‘Campus Life (k24),’ ‘Visanga (K24),’ na ‘Kijakazi Chizi (Star time Swahili) kati ya zingine nyingi.

Katika mpango mzima amefanya kazi na makundi mengi tu ikiwamo Shoebak Production na Geartrix kati ya mengine.

Mwigizaji huyu anapinga tetesi za kwamba wakenya wengi hupenda kutazama filamu za mataifa ya kigeni.

Anatoa mwito kwa Serikali ya Kenya inastahili kuweka mikakati kabambe kuhakikisha vyombo vya habari zinapeperusha asilimia tisini ya kazi za wazalendo. Kadhalika anasema itakuwa vizuri endapo wataruhusiwa kushuti filamu zao mahali popote hapa nchini hasa kwenye majengo ya serikali.

Kwa wasanii wote wanaofanya vizuri anasema anaweza kufanya kazi nao. Anatoa mfano na wachekeshaji wawili wa Tanzania akiwamo Oka Martin na Carpoza anaposema huvutiwa na kazi yao.

SHAMBA LAKE

Mwigizaji huyu anasema hupitia changamoto nyingi tu hasa kutoaminika na maprodusa hali ambayo huchangia kunyimwa nafasi za kuigiza.

”Nyakati zingine huwa tunafanya kazi tulielewa tutalipwa lakini mwisho wa siku huondoka mikono mitupu,”’ alisema na kuongeza kwamba produsa wanastahili kuelewa pia nao wana mahitaji katika maisha yao. Anadokeza kuwa uigizaji ndio shamba lake linamsaidia kuweka mkate kwa meza.

USHAURI

Msanii huyu anashauri wenzake wanaokuja kwamba wawe na subira pia lazima wawe wenye roho ngumu maana bila hilo kamwe hawawezi kufika mbali katika tasnia ya filamu.

Kadhalika amesema lazima wajiandae kwa ushindani maana wapo ulingo huo umefurika waigizaji wengi wanaume na wanawake wanaosaka nafasi ambazo ni adimu nchini.