Didmus atoweka na umati wa Wangamati

Didmus atoweka na umati wa Wangamati

NA BRIAN OJAMAA

KIZAAZAA kilishuhudiwa katika eneo la Chebukwabi eneobunge la Kimilili katika shughuli iliyoongozwa na Gavana wa Bungoma, Bw Wycliffe Wangamati, mbunge wa eneo hilo Didmus Barasa alipoondoka na umati wote alipozuiwa kuhutubu.

Hafla hiyo ilikuwa ya kumkaribisha nyumbani mwana wa kiume wa Bi Mary Kosuya kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Msimamizi wa Wadi katika serikali ya Bw Wangamati.

Bi Kosiya ni mfanyakazi wa Afisi ya Hazina ya Ustawi wa Eneobunge la Kimilili (NG-CDF).

Akihutubia umati huo umbali kwa mita 300 kutoka mahala pa sherehe, Bw Barasa alipuuzilia mbali hatua ya Afisa Mkuu wa serikali ya Kaunti ya Bungoma, Patrick Wandili kumnyima nafasi ya kuhutubu.

Mbunge huyo alikariri kuwa Kimilili ni kwao na hatakubali kutishwa na mtu yeyote.

“Mimi ni mzaliwa wa eneobunge la Kimilili ambako ninahudumu kama mbunge. Mtu kutoka nje (akimrejelea Bw Wandili) hawezi kuja hapa kunitisha. Ningetaka kumwambia Gavana Wangamati kuwa hatapata hata kura moja kutoka Kimilili,” Bw Barasa akasema kwa hasira.

Mbunge huyo mbishani aliwataka wapigakura wa eneobunge hilo kumpigia kura Spika wa Seneti Kenneth Lusaka ili amwondoe mamlakani Bw Wangamati.

“Wangamati amewafeli wakazi wa Bungoma kwa uongozi mbaya na anafaa kuondolewa mamlakani,” Bw Barasa akasema.

Mbunge huyo anayeegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA) alisema kuwa ni Bw Lusaka pekee anayetoka eneobunge la Kimilili ambaye anaweza kuiwezesha Bungoma kufikia upeo wa maendeleo.

“Tumesalia na siku 45 pekee kabla ya wapiga kura kuelekea debeni kuwachagua viongozi wanaowataka. Nawaomba tufanya uamuzi wa busara kwa kuwachagua viongozi wanaofaa,” akasema Bw Barasa.

Aidha, aliwataka wakazi wa Kimilili kumpa nafasi nyingine aweze kuwahudumia kama mbunge wao kwa misingi ya rekodi yake nzuri ya maendeleo.

“Kazi ambayo nimefanya hapa ndani ya miaka mitano kama mbunge haiwezi kulinganishwa na kazi ambayo imefanywa na wale walionitangulia,” Bw Barasa akasema.

Mbunge huyo aliwahimiza wanasiasa kuzingatia kanuni zilizowekwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kuendesha kampeni za habari.

“Sisi katika muungano wa Kenya Kwanza hua tunahubiri amani na utangamano katika kampeni zetu. Lakini wapinzani wetu wa Azimio la Umoja ndio husababishwa fujo na vita baada ya kung’amua kuwa tutawashinda,” Bw Barasa akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

KRA yazindua mfumo wa kuunganisha risiti za biashara na...

Mwili wa mchimba dhahabu wapatikana baada ya miezi 8

T L