Siasa

Didmus Barasa amtaka Uhuru kumpigia debe Raila uenyekiti AUC

March 6th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

MBUNGE wa Kimilili Didmus Barasa sasa anamtaka Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuvunja kimya chake na kutangaza wazi ikiwa anaunga mkono azma ya kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga kuwania kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kulingana na Bw Barasa, wandani wake Bw Odinga ambao ni Bw Kenyatta, kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na mwenyekiti wa chama cha Kanu Gideon Moi, wanafaa kumuunga mkono kikamilifu katika azma yake.

Pia anasema wanafaa kufuata nyayo za Bw Odinga kwa kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto kupiga jeki shughuli za maendeleo.

Akihutubu kwenye halfa ya kuzindua basari ya takriban Sh47 milioni katika shule ya wasichana ya St Catherene, Chepnyal iliyoko Kaunti ya Pokot Magharibi, mbunge huyo wa United Democratic Alliance (UDA) alipuuzilia mbali muungano mpya ambao unasukwa na Mbw Kalonzo na Moi ili kufufua uliokuwa muungano wao wa One Kenya Alliance (OKA)  ili wakakabiliane naye Rais Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka wa 2027.

“Tulimshinda Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 na bado ana majeraha, hajapona. Sasa wao itakuwa rahisi kuwatafuna. Nasikia eti ‘Baba’ akitoka wanajipanga kukabiliana na Rais Ruto lakini wafahamu hiyo ni ndoto ya mchana,” akasema Bw Barasa.

Mbunge huyo alimpongeza Rais Ruto kwa kumuunga mkono Bw Odinga.

“Ametafutiwa kazi na hiyo ni hatua nzuri,” akasema Bw Barasa.

Rais Ruto na serikali yake inamuunga Bw Odinga kuwania kiti cha uenyekiti wa AUC.

Majuzi, Rais Ruto na mwenzake wa Uganda Yoweri Mseveni walifanya mazungumzo nchini Uganda kwa kile ambacho kilionekana kuanza mipango za kumfanyia kampeni Bw Odinga ambaye anasifika pakubwa kwa siasa za upinzani nchini Kenya.

Aidha Bw Kalonzo, kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa na kinara wa chama cha Usawa Kwa Wote  Mwangi wa Iria, walikutana na Bw Moi katika boma lake la Kabarak mjini Nakuru kujadili jinsi ya kuchukua nafasi yake Bw Odinga kwenye muungano wa Azimio kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa 2027.

Haya yanajiri huku kukiwa na minong’ono kuwa baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wanapinga hatua ya Bw Odinga kuwania uenyekiti AUC wakimpendekeza Bw Kenyatta kuwa ndiye anafaa kuwania nafasi hiyo.

Hata hivyo Bw Kenyatta amesalia kimia kuhusu suala hilo.

[email protected]