Didmus Barasa asema amegura siasa za wilbaro kuunganisha Waluhya

Didmus Barasa asema amegura siasa za wilbaro kuunganisha Waluhya

Na CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kimilili Didmus Barasa ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto ametangaza kuwa atajiondoa kwa muda kutoka siasa za vuguvugu la hasla ili kusaka umoja wa Waluhya.

Akiongea Jumapili nyumbani kwake katika eneo la Nasianda, kaunti ya Bungoma, Bw Barasa hata hivyo alifafanua kuwa hajagura vuguvugu hilo linaloendelea siasa za kutetea masilahi ya masikini.

“Najiondoa kutoka shughuli za kundi la hasla kwa miezi minne ili nipate wakati wa kuleta pamoja makundi kinzani ya kisiasa katika eneo pamoja na magharibi. Naamini kuwa jamii ya Mulembe inafaa kuongea kwa sauti moja tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema.

“Lakini ningependa kubaini kuwa sijajiondoa kama mwanachama wa vuguvugu la hafla ambalo linalenga kuimarisha maisha na chumi za wanyonge katika jamii,” Bw Barasa akaeleza.

Likizo hiyo ya kutojihusisha na mikutano ya kisiasa inatafsiriwa kama pigo kwa Naibu wa Rais, Dkt Ruto na ambaye amekuwa akiendesha kampeni maeneo mbalimbali nchini kusaka kura kuingia Ikulu 2022.

Bw Barasa amekuwa miongoni mwa wabunge kutoka Magharibi mwa Kenya ambao wamekuwa wakipigia upatu umaarufu wa Dkt Ruto eneo hilo.

Wachanganuzi wanasema kuwa Bw Barasa yuko njiani kujiondoa kutoka kwa kambi ya Dkt Ruto baada ya kung’amua kuwa uwepo wake huku kutachangia apoteze kiti chake.

“Bw Barasa, sawa na wandani wengine wa Naibu Rais kutoka magharibi wameng’amua kuwa wakazi wengi sasa wamechangamkia muungano kati ya Mudavadi na Wetang’ula wala sio Ruto. Barasa amegundua kuwa akiendelea kujinasibisha na Naibu Rais atapateza kiti chake cha Kimilili, 2022,” anasema Herman Manyora ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

“Hivi karibuni utawasikia wengine kama vile Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Malulu Injendi (Malava) kati ya wengine wakigura kambi ya Ruto,” akaongeza mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Vile vile, inasemekana kuwa wandani wa Dkt Ruto kutoka jamii ya Waluhya wameingiwa baridi ya kisiasa, baada ya kung’amua kuwa ushirikiano kati ya Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula unaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

Ufinyu wa ushawishi wa Dkt Ruto katika eneo la magharibi ulidhihirika majuzi pale wagombeaji wa chama chake, United Democratic Alliance (UDA) walipobwagwa katik chaguzi ndogo za Kabuchai (Bungoma) na Matungu (Kakamega).

Ford Kenyatta ilihifadhi kiti cha Kabuchai kupitia Bw Majimbo Kalasinga huku Oscar Nabulindo wa ANC akitwa kiti cha Matungu.

Katika vurugu zilizozuka katika uchaguzi mdogo wa Kabuchai, Bw Barasa ni miongoni mwa wabunge wanne waliokamatwa kwa tuhuma za kuchochea fujo hizo. Wengine walikiwa Nelson Koech (Belgut), Wilson Kogo (Chesumei) na Seneta wa Nandi Samson Cherargei.

Baadaye Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i aliamuru wanne hao kupokonywa walinzi wao na leseni za kumiliki bunduki. Walishtakiwa katika mahakama ya Bungoma na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu, kila mmoja.

Kesi dhidi yao itasikizwa mnao Aprili 5, 2021.

Kando na Mudavadi na Wetang’ula, Waziri wa zamani Mukhisa Kituyi ni mwanasiasa mwingine kutoka magharibi mwa Kenya ambaye ametangaza nia ya kuwania urais, 2022.

You can share this post!

Korongo Ziwa Bogoria wazidi kuangamia

Hatimaye mitihani yaanza kwa KCPE