Michezo

DILI YANUKIA: Dili ya Dybala kwenda Manchester United yakaribia kuiva

August 2nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MPANGO wa Manchester United na Juventus kubadilishana wachezaji Paulo Dybala na Romelu Lukaku unakaribia kuiva, tetesi nchini Italia zinasema.

Mkurugenzi wa michezo wa Juventus, Fabio Paratici anaaminika ametua nchini Uingereza kwa mazungumzo na United pamoja na mawakala wa washambuliaji hawa wawili “ili kufikia mapatano na kukamilisha ubadilishanaji”.

Kulingana shirika la habari la Sky, mpango huo “ni kama umeshakamilika” na kuwa mpira sasa uko upande wa Dybala kukubali kuhama.

Dybala anataka mshahara wa karibu Sh1.1 bilioni kila mwaka ndiposa amwage wino United.

Ubadilishanaji wa wachezaji Dybala na Lukaku unaonekana unakaribia kufaulu, ingawa “mashetani wekundu” United watalazimika kumpa donge nono ili kumshawishi Dybala kuachana na soka ya Klabu Bingwa Ulaya kwa kuhamia uwanjani Old Trafford.

Na tovuti ya talkSPORT imefichua kuwa Dybala anataka sharti hilo litimizwe kwanza. “Inaaminika kuwa Dybala anataka mshahara wa Sh1.1 bilioni kila mwaka.

“Atakuwa akipatia kisogo soka ya Klabu Bingwa Ulaya kwa miezi 12 kwa kuondoka Juventus ili kujiunga na United.

“Tunaambiwa kuwa Lukaku, ambaye moyo wake ulikuwa tayari kujiunga na Inter Milan, amekubaliana na Juventus kujiunga nayo, yeye anatamani sana kuondoka Old Trafford.

“Hata hivyo, ikiwa United inataka Dybala, italazimika kulipa fedha nyingi,” tovuti hiyo inasema.

Dybala anasemekana anataka mshahara unaozidi ule wa kiungo Mfaransa Paul Pogba anaopata ndiposa ajiunge na United.

Raia huyo wa Argentina anatarajia mshahara wa Sh43.8 milioni kutoka kwa United. Waajiri wake wa sasa Juve wamemweleza kuwa hatatumiwa nao kama chaguo la kwanza msimu ujao wa 2019-2020 na watafurahia akihama.

Pogba alilazimika kukubali kukatwa mshahara wake wa kila wiki wa Sh37.5 milioni kwa asilimia 25 baada ya United kukosa kufuzu kushiriki Klabu Ulaya.

Hiyo ndiyo sera ya klabu ya United, lakini Dybala na mawakala wake waliambia viongozi wa United kuongeza kitu kizuri juu ya mshahara wa kila wiki wa Pogba mazungumzo yalipoanza juma hili.

Kuongezwa

United pia iliongezwa mshambuliaji mzoefu wa Croatia, Mario Mandzukic, 33, kama sehemu ya mpango huo.

Hata hivyo, lengo kubwa limekuwa kulainisha makubaliano na Dybala, 25.

United itatoa mwangaza zaidi kuhusu Mbelgiji Lukaku kuelekea mjini Turin mara tu matakwa ya kibinafsi yatakubalika na Dybala.

Lukaku, 26, alirejea katika uwanja wa United wa kufanyia mazoezi wa Carrington juzi baada ya mazungumzo ya kuhamia Juve kukosa kuzaa matunda jijini London.

Kocha wa United, Ole Gunnar Solskjaer anataka hali ya Lukaku itatuliwe juma hili kuhakikisha anapata muda wa kutafuta kizibo chake.

Hata hivyo, hali hii imekuwa ikijivuta polepole, huku Dybala akishikilia kuwa matakwa yake yatimizwe kwanza na kumuacha Lukaku katika hali isiyoeleweka.

Mvutano huu huenda ukaruhusu Inter Milan kutafuta nyota huyo wa zamani wa Everton.

Inter imeshuhudia ofa yake ya Sh6.7 bilioni ikikataliwa na iko tayari kuiimarisha hadi Sh8.1 bilioni.