Michezo

DIMBA: Dejan, kifaa cha Juve kinachowania tuzo ya ‘Golden Boy’

November 2nd, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

DEJAN Kulusevski ni mmoja wa wanasoka makinda ambao kazi yao uwanjani inatambulika katika safu ya katikati barani Ulaya.

Kulusevski ni mali ya Juventus baada ya miamba hao wa Italia kumnyakua kwa Sh4.5 bilioni kutoka Atalanta mnamo Januari 2 mwaka 2020 kwa kandarasi ya miaka minne na nusu.

Kiungo huyu Mswidi mwenye asili ya Macedonia alizaliwa Aprili 25 mwaka 2000. Anasherehekea siku moja ya kuzaliwa na beki Mfaransa Raphael Varane,27, anayechezea Real Madrid na kipa nambari moja wa Algeria Rais M’Bolhi, 34.

Kulusevski, ambaye anafahamika kwa jina la utani kama Shady, aliibuka mchezaji bora chipukizi wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu uliopita wa 2019-2020 na pia kutajwa katika timu ya msimu ya Serie A ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 22 baada ya mchango mkubwa kwa timu ya Parma alikokuwa kwa mkopo. Alifungia Parma mabao 10 na kumega pasi nane zilizozalisha magoli katika msimu huo.

Mchezaji huyo alianzia soka yake katika klabu ya Brommapojkarna aliyowahi kuchezea beki Mkenya David ‘Cheche’ Ochieng’. Kulusevski alikuwa Brommapojkarna kwa misimu 10 kabla ya kujiunga na timu ya chipukizi ya Atalanta mwaka 2016 alikomezewa mate na Juventus.

Mchezo wake wa kuridhisha umeshuhudia Kulusevski akitiwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo ya Golden Boy ambayo inatolewa na waandishi wa michezo barani Ulaya kwa mchezaji bora chipukizi barani humo kila mwaka. Mshindi wa tuzo hiyo mara nyingi huaminika atafikia kiwango cha kuwa supastaa uwanjani.

Washindi wa tuzo hiyo ya kifahari tangu ianzishwe mwaka 2003 inajumuisha Rafael van der Vaart, Wayne Rooney, Lionel Messi, Cesc Fabregas, Sergio Aguero, Anderson, Alexandre Pato, Mario Balotelli, Mario Gotze, Isco na Paul Pogba. Pia, kunao Raheem Sterling, Anthony Martial, Renato Sanches, Kylian Mbappe, Matthijs de Ligt na Joao Felix.

Kulusevski amejizolea sifa kwa kuwa kiungo ambaye ni mweledi katika kudhibiti mpira, kupiga chenga na kuchanja pasi za uhakika. Alifunga mabao matamu dhidi ya Bologna na Brescia msimu uliopita kuonyesha kuwa ukimwachia nafasi utaishia kujilaumu. Pia, ni mzuri katika kuvunja mashambulizi ya wapinzani na kuunda nafasi.

Mshindi wa tuzo ya Golden Boy 2020 atajulikana Desemba 14 baada ya waandishi wa michezo kutoka Bara Ulaya kupiga kura.

Kulusevski anawania tuzo hiyo dhidi ya Waingereza Bukayo Saka (Arsenal), Callum Hudson-Odoi (Chelsea), Phil Foden (Manchester City), Mason Greenwood (Manchester United), Mreno Fabio Silva (Wolverhampton Wanderers) na Mhispania Ferran Torres (Manchester City).

Mhispania Ansu Fati (Barcelona), Sergino Dest (Barcelona/Amerika) na raia wa Brazil Rodrygo na Vinicius Junior (Real Madrid), Mwamerika Sergino Dest (Barcelona), Alphonso Davies (Bayern Munich/Canada), Erling Braut Haaland (Borussia Dortmund/Norway) na Mwingereza Jadon Sancho (Borussia Dortmund) pia wako katika orodha ya wachezaji wanaowania tuzo hiyo.

Mwitaliano Sandro Tonali (AC Milan), Jonathan David (Lille/Canada), Mitchel Bakker (PSG/Uholanzi), Eduardo Camavinga (Rennes/Ufaransa), Ryan Gravenberch (Ajax/Uholanzi) na Dominik Szoboszlai (RB Salzburg/Hungary) wanakamilisha orodha hiyo ya wawaniaji.

Juventus almaarufu ‘Old Lady’, wanalipa Kulusevski mshahara wa Sh321.4 milioni kila mwaka (Sh2.05 milioni kila wiki).

Katika msimu huu ambao bado ni mbichi, Kulusevski amesakata michuano mitano akipachika mabao mawili.