DIMBA: Huyu chipukizi En-Nesyri anawindwa kama Mo’ Salah

DIMBA: Huyu chipukizi En-Nesyri anawindwa kama Mo’ Salah

Na GEOFFREY ANENE

YOUSSEF En-Nesyri ni mmoja wa wachezaji chipukizi wanaomezewa mate na timu za kutoka ligi maarufu ya soka duniani, EPL.

Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Morocco huenda akavalia jezi ya West Ham, Manchester United, Liverpool ama Arsenal hivi karibuni akiamua kuwapa kisogo waajiri wake Sevilla.

Amehusishwa na klabu hizo pamoja na Wajerumani Borussia Dortmund wanaomrushia chambo ili kumfanya awe kizibo cha supastaa Erling Haaland, ambaye yuko kwenye rada ya mabwanyenye Manchester City, Chelsea, Paris Saint-Germain na Real Madrid.

En-Nesyri amelinganishwa kimchezo na ‘muuaji’ Mohamed Salah, 28.

Mguu wake hatari ni sawa na ule ambao mshambuliaji huyo wa Misri na klabu ya Liverpool anatumia – kushoto.

Chipukizi huyu, ambaye alizaliwa Juni 1 mwaka 1997 mjini Fes, alianza kukuza mchezo katika akademia ya soka ya Mohammed VI mjini Sale.

Mnamo 2015, alijiunga na klabu ya Malaga nchini Uhispania kwa soka ya kulipwa ambapo alinunuliwa kwa kitita Sh16.3 milioni kutoka akademia ya Mohammed VI mnamo 2015.

Alianzia timu ya pili ya Malaga (Malaga B) akifunga mabao sita katika mechi sita na kupandishwa kwa haraka kuingia timu ya watu wazima.

Alijumuishwa katika kikosi hicho na aliyekuwa kocha wa Malaga wakati huo Juande Ramos kwa maandalizi ya Ligi Kuu ya msimu mpya. Alitikisa nyavu mara mbili timu hiyo ikilelemea Algeciras 4-0 Julai 16, 2016.

Kufuatia mchezo wa kuridhisha, En-Nesyri aliamua kuongeza kandarasi yake Agosti 23. Siku tatu baadaye, alisakata mechi yake ya kwanza rasmi akijaza nafasi ya Keko Gontan katika sare ya 2-2 dhidi ya wenyeji Espanyol.

En-Nesyri alikamilisha msimu 2017-2018 kwa mabao manne baada ya kutumiwa uwanjani mara 25. Malaga iliangukiwa na shoka.

Mnamo Agosti 17, 2018, alisaini kandarasi ya miaka mitano na Leganes iliyokuwa La Liga, kwa Sh783 milioni.

Alichezea Leganes michuano 49 na kuifungia mabao 13 katika misimu miwili ya kwanza. Aliandikisha historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka klabu hiyo kupata ‘hat-trick’ kwenye La Liga alipoifungia mabao yote ikishinda Real Betis 3-0 Februari 10, 2019.

Mnamo Januari 16, 2020, Sevilla ilinyakua En-Nesyri kutoka Leganes kwa ada ya uhamisho ya Sh3.2 bilioni. Alisaini kandarasi itakayokatika Juni 2025. Leganes ilikuwa imeshushwa ngazi.

Kabla ya wikendi iliyopita, En-Nesyri alikuwa ametandazia Sevilla jumla ya mechi 63. Hakuwa na mchango mkubwa katika msimu wake wa kwanza wa 2019-2020 alipopachika jumla ya mabao sita katika mechi 26 kwenye mashindano ya Ligi ya Uropa, Copa del Rey na La Liga.

Alionjeshwa dakika tano za muda wa kawaida na sita za majeruhi katika fainali ya Ligi ya Uropa ya msimu huo ambapo Sevilla iliweka rekodi mpya ya mataji mengi (sita) baada ya kukung’uta Inter Milan 3-2.

Hata hivyo, amejitokeza kutesa barani Ulaya msimu huu wa 2020-2021.

Mchango wake katika timu hiyo ya kocha Julen Lopetegui kwenye La Liga mwezi Januari ulishuhudia akitawazwa Februari 5 kuwa mchezaji bora wa mwezi huo.

Alibuka bora Januari kutoka kwa orodha ya wagombeaji sita – Luis Suarez, Toni Kroos, Frenkie de Jong, Pau Torres, Sergio Canales na Roger Marti.

Mwezi huo, En-Nesyri alifungia Sevilla mabao yote katika ushindi wa Real Sociedad 3-2 na Cadiz 3-0 uwanjani Ramon Sanchez Pizjuan na la ufunguzi wakilemea wenyeji Alaves 2-1.

Anaongoza ufungaji wa mabao ya Sevilla kwenye La Liga msimu huu. Anayemkaribia Sevilla ni raia wa Argentina Lucas Ocampos (manne).

En-Nesyri, ambaye anapokea mshahara wa Sh7.4 milioni kila wiki, amefungia Sevilla mabao manne kwenye Klabu Bingwa Ulaya msimu huu. Hakuona lango Seville ikipoteza 3-2 dhidi ya Borussia Dortmund nchini Uhispania mnamo Februari 17. Huenda akawa mwiba timu hizi zitakaporudiana hapo kesho kuamua nani kati yao anaingia robo-fainali.

Kimataifa, En-Nesyri amewakilisha Morocco mara 21. Alichezea Atlas Lions kwenye Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2017 na 2019 na Kombe la Dunia mwaka 2018.

Baadhi ya sifa zake nzuri ni kuwa ana nguvu, ukatili katika kukamilisha mashambulizi na si mchache katika kuwania mipira ya hewani.

Ulegevu wake mkubwa ni mazoea ya kujenga kibanda katika himaya ya wenyewe. Katika michuano yake ya kwanza 24 kwenye La Liga msimu huu, aliotea mara 16.

You can share this post!

Ajuta kupeleka kesi kwa wakwe

Uhuru ataweza Raila na Ruto?