DIMBA: Huyu Jo ndiye andazi moto la uhamisho 2021

DIMBA: Huyu Jo ndiye andazi moto la uhamisho 2021

Na GEOFFREY ANENE

JONATHAN Christian David ni mmoja wa wanasoka matata wanaotarajiwa kuwaniwa sokoni kama mpira wa kona.

Kipindi kirefu cha uhamisho kimeratibiwa kufunguliwa Juni 9 nchini Uingereza na Julai 1 nchini Ujerumani, Ufaransa, Uhispania na Italia.

Mshambuliaji huyu wa Lille ni chipukizi wa taifa la Canada. Alichangia pakubwa katika kampeni ya Lille kutesa kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa ya msimu 2020-2021. Mara ya mwisho Lille kushinda ligi ulikuwa msimu wa 2010-2011. David maarufu kama Jo, alifunga mabao 13 katika michuano 37 ligini msimu huu.

Katika mchuano wa kufunga msimu dhidi ya Angers, Jo alitikisa nyavu mara moja na kisha kupata penalti iliyofungwa na Burak Yilmaz. Lille ililemea Angers 2-1 na kumaliza juu ya jedwali.

Mabwanyenye Paris Saint-Germain, ambao wanajivunia kuwa na masupastaa Neymar na Kylian Mbappe, walikuwa wametawala Ufaransa kwa misimu mitatu mfululizo.

Kwa kupata idadi hiyo ya mabao, Johari ya Canada aliingia katika daftari la kumbukumbu kama raia wa kwanza wa taifa hilo kufunga mabao mengi katika ligi tano kubwa za Bara Ulaya (Uingereza, Ufaransa, Uhispania, Italia na Ujerumani). Alifuta rekodi ya mabao 11 ambayo Tomasz Radzinski aliweka msimu 2002-2003 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza akichezea Everton.

Jo alizaliwa Januari 14 mwaka 2000 mjini New York nchini Amerika. Ana asili ya Haiti. Kifunguamimba huyo kutoka familia ya watoto wawili alianza kupenda soka akiwa katika shule ya msingi ya Louis Riel. Akiwa katika shule hiyo ya umma aliota kusakata soka ya malipo barani Ulaya.

Rekodi zinaonyesha kuwa alipitia mikononi mwa vituo vya kukuza talanta vya Gloucester Dragons, Ottawa Gloucester, Ottawa Hornets na Ottawa Internationals nchini mwake kati ya 2011 na 2018.

Alifeli majaribio katika klabu nyingi zikiwemo Red Bull Salzburg nchini Austria na Stuttgart nchini Ujerumani kabla ya kualikwa na Gent nchini Ubelgiji na kupita mtihani akiwa na umri wa miaka 16.

Kipindi chake cha kwanza cha mazoezi na Gent kilikuwa kibovu. Jo alinukuliwa akisema kuwa alidhani Gent ingemtema baada ya kipindi hicho, lakini ilimpa fursa nyingine. Aliridhisha kiasi cha kocha wake kumueleza kuwa amejaliwa na talanta nzuri ya kuwa mchezaji wa soka.

Kwa sababu Gent ni klabu ndogo barani Ulaya, David alikuwa na mpango kabambe wa kuvutia macho ya ligi kubwa kwa kumiminia wapinzani mabao.

Miungu wa soka walisikia maombi yake ya kujinadi kupitia ufungaji wa mabao. Alipopewa fursa na Gent kuonyesha maarifa yake uwanjani, alifunga jumla ya mabao sita katika mechi zake nane za kwanza kati ya Agosti 4 na Agosti 30 mwaka 2018 ligini na Ligi ya Uropa.

Ukatili huo wake dhidi ya makipa ulishuhudia Gent ikishawishika kuongeza kandarasi hadi 2023 baada ya klabu kubwa kuanza kumzingira kama papa mawindoni. Alikamilisha msimu huo wa 2018-2019 akiwa amefungia Gent mabao 37 katika michuano 83 katika mashindano yote.

Jo pia hakuachwa nyuma katika kutoa huduma zake kwa timu ya taifa. Alinyeshea timu pinzani magoli na kuibuka mfungaji bora kwenye Kombe la Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (CONCACAF) Gold Cup alipotikisa nyavu mara sita. Canada ilibanduliwa na Haiti katika robo-fainali ya dimba hilo. Alitajwa kuwa mwanasoka bora wa mwaka mwanamume nchini Canada mwaka 2019.

Alikuwa katika kikosi cha Canada kilichopiga majirani Amerika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 34 katika Ligi ya CONCACAF mnamo Oktoba 2019.

Mkazi huyo wa mji wa Ottawa, ambaye alikataa mwito wa kuchezea Amerika, alijiunga na Lille mnamo Agosti 11 mwaka jana.

Kabla awe mali ya Lille kwa Sh4.1 bilioni, alikuwa amehusishwa na uhamisho hadi Arsenal, United, Everton, Leeds, Porto, Ajax, Inter Milan, Lyon, Borussia Dortmund, Borussia Monchengladbach na Bayer Leverkusen.

Nguvu za Jo, anayemezewa mate na Arsenal na Manchester United, si katika ubunifu, bali anapenda kutumia nguvu zake za kimwili na kasi yake pamoja na kuhangaisha mabeki kwa mikimbio ndani ya kisanduku.

Aidha, yeye ni mweledi katika kufanya uamuzi uwanjani. Anaweza kucheza katika nafasi yoyote katika idara ya ushambuliaji na hata kama kiungo mshambuliaji.

Mchezo wake unakaribiana sana na ule wa Marcus Rashford (Manchester United) na Mkorea Heung-min Son.

Tangu aanze kuchezea timu ya taifa ya watu wazima ya Canada mwaka 2018, Jo ameifungia mabao 11 katika michuano 12. Macho yatakuwa kwake mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 za eneo la CONCACAF zitakaporejea juma hili. Alikosa michuano miwili iliyopita ambazo Canada ililipua Bermuda 5-1 na Cayman 11-0 mwezi Machi kutokana na masharti makali ya Ufaransa dhidi ya usafiri baada ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.

Kandarasi ya Jo katika klabu ya Lille itakatika Juni 2025. Hii inamaanisha kuwa klabu yoyote inayomtaka wakati huu italazimika kulipa ada kubwa ya uhamisho. Mchezaji huyu hupokea mshahara wa Sh5.8 milioni kila wiki (Sh302 milioni kila mwaka).

You can share this post!

Uhuru aangusha minofu kwa Raila

Karua apendekeza wakati wa uchaguzi kuwe na maafisa maalum