DIMBA: Jules Kounde ni kisiki kisichovuja ligini Uhispania

DIMBA: Jules Kounde ni kisiki kisichovuja ligini Uhispania

Na GEOFFREY ANENE

JULES Oliver Kounde ni mmoja wa mabeki matata kambini mwa Sevilla.

Mfaransa huyu mwenye asili ya Benin anafanya kazi safi katika klabu hiyo ya Uhispania, huku sifa zake zikitambulika na klabu kubwa nchini Uingereza.

Ni sifa ambazo zimemfanya kumezewa mate na mashetani wekundu wa Manchester United, wanabunduki wa Arsenal na Tottenham Hotspur ya Jose Mourinho.

Kounde amehusishwa pia na Real Madrid. Aliwahi kutafutwa na mabwanyenye Manchester City katika kipindi kirefu cha uhamisho mwaka 2020, lakini hawakuelewana bei.

Tetesi kutoka ugani Old Trafford kule kwa Man-United zinasema kuwa kocha Ole Gunnar Solskjaer tayari ameshapanga jinsi atakavyomtumia.

Anataka ashirikiane na beki ghali duniani Harry Maguire, na kuwachochea Victor Lindelof na Eric Bailly kujituma zaidi.

Cafu, anavyofahamika kwa jina la utani kutokana na uchezaji wake unaokaribiana na shujaa huyo Mbrazil, alizaliwa katika jiji la Paris nchini Ufaransa mnamo Novemba 12, 1998.

Mamake ni Mfaransa huku babake akiwa anatokea Benin. Alilelewa na mamake kuanzia umri wa mwaka mmoja katika mtaa wa Landiras viungani mwa mji wa Bordeaux.

Kounde alianza soka akiwa na umri wa miaka mitano kwenye akademia ya Fraternelle de Landiras, ingawa mamake alimsisitizia umuhimu wa masomo.

Alijaribu kucheza katika idara zote uwanjani kabla kuamua kuwa kipa na kisha kuridhika na nafasi ya beki.

Ripoti nchini Ufaransa zinasema hakupenda kupoteza mechi.

“Sikuwa mtoto mzuri kwa mamangu kwa sababu sikutaka kuongeleshwa naye wakati tumepoteza mechi. Nakumbuka nikiwa miaka tisa nilimkosea heshima kwa kumpiga mateke miguuni baada ya timu yangu kupoteza,” alisimulia shirika moja la habari hadithi ya safari yake ya uchezaji wake.

Tabia hiyo ilipozorota, mamake alitafuta mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia ambaye alimshauri ajibu mateke ya mwanawe kwa kumrushia pia mateke. Ilikuwa suluhu rahisi ambayo ilizaa matunda kwani hali kati yao iliimarika.

Kounde aliendelea kukuza talanta yake katika akademia ya Cerons (mwaka 2008 hadi 2010) na La Brede (2010-2013).

Alizamia soka kabisa baada ya kufanyiwa majaribio ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 13, kwenye kituo cha kukuza talanta cha klabu ya Bordeaux na kupita.

Mwanzoni alipata ugumu kupiga hatua kisoka sababu hakupenda kuwasiliana na watu. Akalazimishwa kufungua roho na kukuza urafiki wa ndani na nje ya uwanja.

“Niliambiwa kuwa bila kufanya hivyo wachezaji wenzangu walihisi kwamba mimi si mmoja wao”.

Kounde alitwikwa majukumu ya unahodha ili kumlazimu azungumze na wachezaji wenzake. Ulikuwa muujiza ambao ulimsaidia kuimarika pakubwa kimawasiliano na pia kupunguza hasira.

Kijana huyu mdogo alichangia pakubwa katika Bordeaux kushinda mechi 24 kati ya 26 wakati klabu hiyo ikitwaa taji la chipukizi. Alianza maisha yake katika timu ya watu wazima ya Girondins Bordeaux kwa kishindo msimu 2017-2018, akiibukia kuwa mmoja wa mabeki wazuri katika Ligi Kuu ya Ufaransa.

Chini ya kocha Gus Poyet, mchezo wake wa kuvutia katika nusu ya pili ya msimu huo ulimfanya kutafutwa na klabu nyingi kubwa.

Alichezea Bordeaux jumla ya michuano 70 akipachika mabao manne na kumega pasi moja iliyozalisha goli.

Kounde aliondoka Bordeaux na kujiunga na Sevilla, ya kocha Julen Lopetegui, kwa kandarasi ya miaka mitano kwa dili ya Sh3.3 bilioni mnamo Julai 3, 2019.

Mafanikio yake mengi amepata akiwa uwanjani Ramon Sanchez Pizjuan.

Alishinda taji la Ligi ya Uropa wakati Sevilla ilinyamazisha miamba wa Italia, Inter Milan, kwa magoli 3-2 msimu 2019-2020.

Pia, aliwezesha Sevilla kuingia Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu 2020-2021 ilipokamilisha La Liga katika nafasi ya nne.

Beki huyu amechezea Sevilla zaidi ya mechi 70 zikiwemo 38 katika mashindano yote msimu huu.

Sifa yake imekuwa ikiimarika, na pia bei. Hata hivyo, ripoti zinasema Sevilla imeamua kupunguza bei yake kutoka Sh10.6 bilioni hadi Sh7.6 bilioni ili kurahisisha uhamisho wake.

Kounde amechezea timu ya taifa ya Ufaransa ya wachezaji wasiozidi umri wa 21 michuano minne.

Alifahamu kuwa mwenye asili ya Benin babake alipojitokeza akiwa na miaka 16 ili kuzungumza naye. Mzazi huyo alimuomba aichezee Benin, lakini Kounde alikuwa tayari ameamua kuwakilisha Ufaransa kimataifa.

Nyota huyu chipukizi anapokea mshahara wa Sh10.6 milioni kila wiki.

Ana kibarua kigumu kufikia kiwango cha Marcos Evangelista de Morais, almaarufu kama Cafu. Raia wa Brazil huyo mwenye umri wa miaka 50 anashikilia rekodi ya kuchezea Samba Boys mechi nyingi.

Beki huyo wa pembeni kulia wa zamani wa AC Milan, alishinda Kombe la Dunia mwaka 1994 na 2002 miongoni mwa mafanikio mengine.

You can share this post!

Pasta afokewa kupendelea vipusa

Pigo Ruto akipoteza ‘jenerali’