Makala

DIMBA: Kimya cha Mourinho na Allegri kinarindima Manchester United, Madrid na Spurs

October 14th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MIEZI 10 imepita tangu Jose Mourinho afutwe kazi na Manchester United uwanjani Old Trafford.

Mourinho na Massimiliano Allegri aliyeagana na Juventus mwishoni mwa msimu uliopita ni miongoni mwa wakufunzi wa haiba kubwa kwa sasa ambao hawana kazi.

Matarajio ya Olympique Lyon yalikuwa makubwa baada ya mafanikio ya msimu jana uliowashuhudia wakitinga hatua ya 16-bora katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza tangu 2012 na kuambulia nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) chini ya kocha Sylvinho.

Msururu wa matokeo duni ya Lyon kufikia sasa muhula huu ni kiini cha kutimuliwa kwa Sylvinho wiki jana. Kufutwa kwa beki huyo wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Brazil kulitazamiwa kumpa Mourinho au Allegri nafasi ya kupokezwa ukocha wa Lyon.

Ingawa hivyo, inaelekea kwamba huenda Lyon wakamwajiri aliyekuwa kocha wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Ufaransa, Laurent Blanc au mkufunzi wa zamani wa AS Roma, Rudi Garcia.

Mourinho akataa kuifunza Lyon

Mourinho na Allegri walikataa ofa ya kudhibiti mikoba ya Lyon licha ya maarifa yao kuhemewa na Rais wa kikosi hicho, Jean-Michel Aulas.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uhispania, hatua hiyo ya Mourinho inazidisha tetesi zinazomhusisha na uwezekano wa kumrithi Zinedine Zidane kambini Real Madrid huku Allegri akipigiwa upatu wa kutua uwanjani Old Trafford kudhibiti mikoba ya Man-United iwapo miamba hao wa zamani wa Uingereza watamtimua Ole Gunnar Solskjaer.

Japo Allegri anahusishwa na mikoba ya Man-United, huenda akahiari kuyoyomea AC Milan kujaza pengo la Marco Giampaolo aliyetimuliwa wiki jana, siku chache baada ya Sampdoria ambayo pia inanogesha soka ya Italia (Serie A) kumpiga kalamu Eusebio di Francesco.

Iwapo Allegri ataelekea AC Milan, nao Man-United wamfute Solskjaer, gazeti la Mirror Sport nchini Uingereza limefichua uwezekano wa kocha wa sasa wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino kutua ugani Old Trafford.

Kiini cha hilo ni kauli ya hivi majuzi ya Pochettino kusisitiza kwamba haogopi kabisa kutimuliwa na usimamizi wa Spurs licha ya matokeo mabovu yanayosajiliwa kwa sasa.

Kuondoka kwa Pochettino kambini mwa Spurs kunatarajiwa kutoa fursa kwa kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Gareth Southgate kuitwaa nafasi yake.

Iwapo Real wataagana na Zidane, Mourinho atakuwa kileleni mwa orodha ya wakufunzi watakaotua ugani Santiago Bernabeu.

Mwingine ni Antonio Conte wa Inter Milan aliyepigiwa upatu wa kuwa kocha wa kikosi hicho msimu uliopita kabla ya nafasi hiyo kumwendea Julen Lopetegui ambaye baadaye alimpisha Santiago Solari kabla ya Zidane kurejea.