DIMBA MASHINANI: Parklands Simba yajivunia mafanikio makubwa tangu iasisiwe Agosti 2020

DIMBA MASHINANI: Parklands Simba yajivunia mafanikio makubwa tangu iasisiwe Agosti 2020

Na PATRICK KILAVUKA

KLABU ya Parklands Simba maarufu kama Simba United, inasherehekea mwaka mmoja tangu iasisiwe Agosti 2020.

Uga wake wa nyumbani ni ule wa Shule ya Msingi ya Kihara, kaunti ndogo ya Kiambaa.

Imestawishwa mizizi yake kiasi cha kupata mashiko katika Ligi ya Kanda ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) na inanawiri na kupania kupanda ligi. Imo katika za nafasi za tano bora.

Dau lao halizami chini ya uongozi mufti wa kocha Livingstone Wanga ambaye alikuwa katika benchi ya kiufundi ya Mathare United akiwa chini ya kocha Francis Kimanzi kabla kuchukua mikoba ya timu hii.

Mbali na kupokea mafunzo ya ukocha kupitia timu ya Mathare United alikojukumika kisoka kama mchezaji mshambulizi pia.

Wengine ni meneja wa timu Cyprian Asaba ‘Sebby’ na katibu Joseph Lomale.

Msukumo ambao umejenga timu hii umetokana na kukuza talanta.

Kulingana na Asaba, talanta ambazo alikuwa amezitambua akishikilia wadhifa huo katika timu nyingine mtaani Gachie, hakupenda kuziona zikitokomea kwa sababu ya mambo ambayo hayastahiki maishani mwa vijana hao ambao walikuwa wameshika darubini ya maisha na talanta.

Pia, aligundua kwamba kupitia michezo vijana wanaweza kuwa na njia mbadala ya kustahamili changamoto za maisha na hata kujinasua katika visa vya utovu wa nidhamu mtaani na mjini.

“Tumesukumwa kujenga vipawa tunavyoviona mtaani kubadilisha maisha ya vijana na kuwaandalia jukwaa la kujitambua na kujikuza, ” akasema meneja wa timu Asaba ambaye ni tatibu na anayejua fika umuhimu wa michezo kwa afya.

Timu hii yenye wanadimba 22 inaonyesha uwezo wa kusakata boli kwani kufikia kuandikwa kwa makala ilikuwa imecheza michuano 21 na kuzoa alama 36

Matokeo yao mazuri kulingana na wadau yametokana na mazoezi makali, nidhamu na mshikamano mfano wa gundi kwenye timu ambao umechochewa wachezaji kujiamini na kujituma kuinua matokeo matamanifu kwa kutandaza soka ya haiba.

Isitoshe, wachezaji wamevunja kasumba ya ukabila, wameimarisha utangamano na kushikana kwa hali na mali. Fauka na kila wachezaji kupigwa jeki baada ya mchezo kama njia ya kuwatia motisha.

Benchi ya kiufundi ya kikosi cha Parklands Simba (Simba United) ikifuatilia mechi wakati wa pambano lao dhidi ya Red Carpet uwanjani Kihumbuini. Simba ilipata ushindi wa 1-0. Picha/ Patrick Kilavuka

Kando na kushiriki ligi hiyo, timu inaongozwa kushiriki katika vipute kama kigezo kingine cha kujitia makali kwa maandalizi ya michuano ya ligi.

Mfano ni kile cha juzi ambacho kilidhamiwa na mshindi wa uchaguzi mdogo wa Kiambaa John Njuguna wa UDA japo ilipoteza mbele ya Karuri Shooting Stars ilipoichabanga 1-0. Pia, ilishiriki na Dimba la Tim Wanyonyi Super Cup 2020 na kufika nusu fainali.

Ni matamanio yao kwamba miaka mitano hivi, watakuwa wanacheza Ligi ya NSL au kupania hata Ligi ya Primia .

Kwa sasa wadau wanasema ufadhili ungali changamoto hususa wa usafiri za mechi za mbali. Itakuwa furaha ya timu iwapo wadhamini watajitokeza kuishika mkono kudumisha azma ya kuyaweka matumaini ya wanavipaji vya kandanda kuwa hai.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iwaombe radhi wanariadha

KAMAU: UhuRuto wasiturejeshe enzi ya Moi kuhusu urithi