Michezo

DIMBA: Matumaini ya majabali Manchester United kurudia hadhi yao yazama 'baharini'

October 7th, 2019 3 min read

Na MWANDISHI WETU

HISTORIA nzuri ya Manchester United katika soka ya Uingereza na bara Ulaya inawaweka katika ulazima wa kutia fora zaidi ili kuweka hai matumaini ya kurejesha hadhi ya zamani iliyotokana na mazoea ya kunyanyua mataji ya haiba kubwa.

Haya ni kwa mujibu wa kiungo wao matata mzawa wa Uhispania, Juan Mata, 31.

Man-United wamemaliza misimu miwili bila ya kutia kapuni taji lolote kwa sasa.

Ingawa hivyo, Mata anaamini kikosi cha sasa kilichosukwa na kocha Ole Gunnar Solskjaer kina uwezo wa kurejesha kumbukumbu nzuri iliyohusishwa na Man-United katika miaka ya awali.

Man-United wamenyanyua mataji mengi zaidi kuliko kikosi chochocte kingine katika historia ya soka ya Uingereza.

Lakini licha ya kubadilisha makocha mara nne, Man-United hawajafaulu kabisa katika juhudi zao za kujitwalia taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) tangu 2013, mwaka ambapo aliyekuwa mkufunzi wao Sir Alex Ferguson alistaafu rasmi.

Taji la mwisho la haiba kubwa zaidi kwa kikosi hicho kutia kapuni ni la Europa League ambalo walilitwaa mnamo Mei 2017 chini ya kocha Jose Mourinho ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Real Madrid, Inter Milan, Benfica, FC Porto na Chelsea.

Ufanisi huo uliwajia miezi mitatu baada ya kunyakua ubingwa wa Carabao Cup. Solskjaer ni mkufunzi wa tano wa Man-United uwanjani Old Trafford katika kipindi cha hivi karibuni.

Mata anahisi historia hii ni ya kutisha sana hasa ikizingatiwa kwamba Man-United walikuwa thabiti na imara zaidi chini ya Ferguson aliyethibiti mikoba yao kwa kipindi cha miaka 26 na nusu.

David Moyes alikuwa akishikilia usukani wa Man-United wakati Mata aliposajiliwa na kikosi hicho kutoka Chelsea kwa kima cha Sh5.2 bilioni mnamo Januari 2014.

Tangu wakati huo, Mata amenolewa pia na wakufunzi Ryan Giggs, Louis van Gaal, Mourinho na Solskjaer. “Kuwa mchezaji wa Man-United ni kitu spesheli sana. Ni tija na fahari tele kuwa sehemu ya kikosi cha miamba hawa wa soka ya Uingereza. Kwa sasa napania kunyakulia kikosi hiki mataji makubwa zaidi. Hiyo ndiyo zawadi ambayo mashabiki wanastahili kupokea kutoka kwetu,” akasema Mata.

Licha ya kujinasia huduma za beki Aaron Wan-Bissaka, fowadi Daniel James, kipa Joel Pereira na difenda ghali zaidi duniani Harry Maguire, Solskjaer huenda akachochewa zaidi kumtwaa Blaise Matuidi wa Juventus, Bruno Fernandes wa Sporting nchini Ureno na fowadi chipukizi Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund mnamo Januari 2020.

Solskjaer kwa sasa ana ulazima wa kujaza nafasi za Antonio Valencia, Ander Herrera, Romelu Lukaku na James Wilson walioyoyomea LDU Quito (Italia), PSG, Inter na Aberdeen nchini Scotland.

Man-United walipoteza zaidi ya Sh12 bilioni kwa hatua yao ya kuwaajiri makocha watatu tofauti katika jitihada za kuusaka uthabiti waliokuwa wakijivunia zamani chini ya Ferguson.

Kiasi hicho cha fedha kilifichuliwa na Man-United wiki jana baada ya usimamizi kumfidia Mourinho na waliokuwa wasaidizi wake tangu watimuliwe mwishoni mwa mwaka jana.

Kulingana na stakabadhi zilizoanika wazi matumizi ya fedha ya Man-United, miamba hawa wa zamani wa soka ya Ligi Kuu Uingereza (EPL) walitumia zaidi ya Sh2.8 bilioni kumlipa Mourinho na wasaidizi wake katika awamu ya kwanza huku salio la Sh2 bilioni likitarajiwa kumwendea Mourinho peke yake kufikia mwisho wa Novemba 2019.

Fedha hizi zikijumuishwa pamoja na mshahara wa hadi Sh1.7 bilioni ambao Mourinho alikuwa akipokezwa kila mwaka ugani Old Trafford, ina maana kwamba Man-United watakuwa wametumia zaidi ya Sh8 bilioni kumtimua Mourinho.

Louis van Gaal pia aliwahi kupokezwa na Man-United kitita kinono cha fedha baada ya kutimuliwa uwanjani Old Trafford alikohudumu kwa kipindi cha misimu miwili. Mbali na mshahara wa hadi Sh462 milioni ambao Mholanzi huyo alikuwa akitia kapuni kwa msimu, Van Gaal pia alipokezwa Sh504 milioni za ziada baada ya kutimuliwa kwake.

Isitoshe, alitia kapuni marupurupu na bonasi za Sh154 milioni na Sh56 milioni kwa mafanikio yake ya kuwashindia Man-United ubingwa wa Ligi ya Uropa (Eu- ropa League) na Kombe la FA mtawalia.

Van Gaal na wasaidizi wake pia walipokezwa kwa pamoja kima cha Sh700 milioni walipotimuliwa siku mbili baada ya kuwanyanyulia waajiri wao ubingwa wa Kombel la FA. Kijumla, Van Gaal alipokezwa fidia ya hadi Sh3.3 bilioni kabla ya kutengana rasmi na Man-United mnamo Mei 2016.

Ili kuhakikisha kwamba Man-United wanampokeza ujira wake wote, Van Gaal alikataa ofa ya kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Ubelgiji mwishoni mwa 2016.

David Moyes naye alitimuliwa na Man-Utd mnamo 2014 baada ya kukatika kwa miezi 10 pekee katika mkataba wake wa miaka sita ugani Old Trafford. Man-United walilazimika kumfurusha Moyes baada ya dalili zote kuashiria kwamba wasingefuzu kwa kipute cha UEFA katika msimu uliofuata. Kufutwa kwa Moyes kulimvunia Sh498 milioni huku akijipa mgao mwingine sawa na huo kutokana na jumla ya Sh728 milioni ambazo yeye na waliokuwa wasaidizi wake walipokezwa baadaye Agosti 2014.